
Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu
imewaachia kwa dhamana Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Zanzibar), Salum Mwalimu
na wafuasi wengine 18 wa chama hicho baada ya kukaa mahabusu kwa zaidi ya siku
12.
Kiongozi huyo wa Chadema na wafuasi
hao 18 walikuwa wakishikiliwa katika mahabusu za jeshi la polisi kwa tuhuma za
kuandaa na kuhamasisha maandamano na mikutano ya Oparesheni ya chama hicho
iliyopewa jina la UKUTA, ambayo ilipigwa marufuku na jeshi hilo.
Walifanikiwa kupata dhamana baada
ya Hakimu wa Mahakama hiyo kueleza kuwa ameridhia hoja za upande wa utetezi
baada ya kusikiliza pande zote mbili na kubaini mapungufu kwenye maombi ya
upande wa mashtaka.
Awali, Mwendesha mashtaka aliitaka
Mahakama hiyo kuwanyima dhamana washtakiwa hao kwa madai kuwa endapo wataachiwa
wataendelea kufanya kosa hilo.
Hata hivyo, Hakimu alitupilia mbali
maombi hayo akieleza kuwa wameshindwa kuthibitisha pasipo shaka kuwa endapo
washtakiwa hao wataachiwa watafanya tena kosa hilo.
Pia, Hakimu alieleza kukubaliana na
hoja ya washtakiwa hao kuwa hati ya kiapo iliyowasilishwa mahakamani hapo na
mwendesha mashtaka ilikuwa na mapungufu ya kisheria.
“Ninakubaliana na upande wa utetezi
kuwa hati ya kiapo iliyowasilishwa ina mapungufu ya kisheria,” alisema Hakimu
baada kupitia na kugundua kuwa aliyesaini hati hiyo sio anayeonekana kuitoa.
Washtakiwa wote walitimiza masharti
ya dhamana kwa kuwasilisha wadhamini wawili kila mmoja ambaye ataweka dhamana
ya shilingi milioni 3.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman
Mbowe alikuwa miongoni mwa watu waliohudhuria mahakamani hapo na kuondoka na
Salum na wafuasi hao ambao walifikishwa mahakamani hapo awali chini ya ulinzi
mkali. Kesi imeahirishwa hadi Oktoba 4 mwaka huu
No comments:
Post a Comment