
Jeshi la Polisi Wilaya ya Chakechake, Pemba limezuia kufanyika
mkutano na vyombo vya habari wa Chama Cha Wananchi (CUF) uliokuwa umepangwa
kufanyika leo wilayani humo, kupisha ziara ya Rais John Magufuli itakayoanza
leo.
Rais Magufuli anatarajia kuanza leo ziara yake ya kwanza
visiwani humo tangu achaguliwe kuwa Mwenyekiti wa CCM.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Ikulu, Rais
Magufuli atazulu Pemba leo na kesho atakuwa Unguja.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Pemba, Shekhani Mohamed Shekhani
amesema kuwa zuio hilo la mkutano wa CUF ni kwa sababu eneo wanalotarajia
kutumia liko jirani na eneo la uwanja atakaokuwa akihutubia Rais Magufuli.
Hata hivyo, Katibu wa CUF wilaya ya Chake Chake, Saleh Nassor
Juma alilalamikia maamuzi hayo ya Jeshi la Polisi kwa madai kuwa wao walitaka
kufanya mkutano na vyombo vya habari na sio mkutano wa hadhara. Alisema kuwa
tayari walishawaeleza Idara ya Habari Maelezo na waliridhia.
Alisema mkutano huo na waandishi wa habari ulilenga katika kutoa
tamko lao kuunga mkono uamuzi uliochukuliwa na Baraza Kuu la chama hicho
kumsimamisha uanachama aliyekuwa Mwenyekiti wake, Profesa Ibrahim Lipumba
pamoja na viongozi wengine 10.
“Niliwakatalia kwa hoja kwamba mkutano na waandishi wa habari ni
haki yetu ya kikatiba na tulikwishawataarifu watu wa Idara ya Habari Maelezo
juu ya kikao hicho halali ambacho wao pamoja na waandishi wa habari
walithibitisha kuwa watahudhuria,” alisema Nassor.
Idara ya Habari Maelezo ilithibitisha kuwa walikubali kufanyika
kwa mkutano huo wa CUF na vyombo vya habari lakini baadae walipokea taarifa ya
kuahirisha kupisha ugeni wa Rais Magufuli.

No comments:
Post a Comment