Sakata la Kampuni ya Kufua
Umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL), kugeuziwa kibao kwa
kutakiwa kurejesha zaidi ya Dola za Marekani milioni 100 ambazo ni zaidi ya Sh
bilioni 216.2 kwa Shirika la Umeme nchini (Tanesco), limezidi kuchukua sura
mpya baada uongozi wa kampuni hiyo kuibuka.
Kuibuka kwa viongozi hao kumekuja
siku chache baada ya Wakili wa Tanesco, kueleza hatua watakazochukua kuhusu
uamuzi huo baadaya Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Kibiashara (ICSID),
uliotolewa Septemba 12 mwaka huu unaoitaka Tanesco kuilipa Standard Chartered
ya Hong Kong (SCB-HK) Dola za Marekani milioni 148.
Akizungumza na waandishi wa habari
jana jijini Dar es Salaam, Kaimu Mwenyekiti ambaye pia ni Mwanasheria wa
Kampuni wa IPTL, Joseph Makandege alisema hawatambui madai ya Benki
ya Standard Chartered ya Hong Kong (SCB-HK) kama mdai na wala hawana haki kwa
mujibu wa sheria.
Kutokana na hali hiyo alisema
inaungana na Shirika la Umeme nchini (Tanesco) kukata rufaa katika Mahakama ya
ICSID kwani hukumu iliyotolewa ina mapungufu mengi ya kisheria.
Licha ya uamuzi huo Makandege
alisema IPTL haikulipwa kwa kutumia viwango vya zamani bali walilipwa kutokana
na umeme waliouuza kwa Tanesco na si vinginevyo.
Alisema watu wasifanye makosa
kuilipa benki hiyo kwani inachotaka kufanya ni kitendo cha utapeli kwa msukumo
wa kampuni za mabeberu.
“Benki ya Standard Chartered ya
Hong Kong hawastahili kulipwa fedha na Watanzania kwani hawastahili kwa mujibu
wa sheria nasi kama IPTL/PAP hatuwatambui na hawana haki ya kutuzungumzia. Na
ndiyo maana wameamua kukimbia mahakama zetu za ndani na kukimbilia nje, hawa
wana msukumo wa mabeberu wenye nia ovu.
“Kwa uamuzi huu wenye utata
uliotolewa na ICSID ni wazi Standard Chartered walikuwa na nia ovu, ninasema
hivyo kwa sababu tangu Septemba 5, mwaka 2013 suala hili liliamuriwa vizuri
chini ya Jaji Utamwa (John) na IPTL ikashinda kesi na kutwaa uongozi.
“Na hili si la kwanza kwani Aprili
3, 2014 tulifungua shauri namba 60 chini ya Jaji Dk. Fauz Twalib la
kuitaka Mahakama itamke kwamba benki ya Standard Chartered Hong Kong si
wadeni wetu, tena awali waliibuka na hoja kwamba hawasikilizwi na Mahakama zetu
za ndani kwa wakati ambapo shauri hilo lilipangiwa kusikilizwa mfululizo.
“Lakini pia dai letu lingine
tuliomba Mahakama Kuu itupe nafuu ya Standard kutulipa gharama kama fidia ya
Dola za Marekani bilioni 3.240 ambapo hata tuzo waliopewa na ICSID eti wanataka
walipwe Dola za Marekani milioni 148 na kama wakitulipa fedha zetu hata madai
yao yaingia humo nabado kuna fedha nyingine inabidi watupatiwe sisi,”alisema Makandege
Wakili huyo ambaye alikuwa
akizungumza kwa niaba ya mmiliki wa IPTL/PAP, Harbindar Singh Sethi mwenye
makazi yake hapa nchini na Afrika Kusini, alisema licha ya mahakama kutoa
uamuzi wataendelea kusimamia uamuzi huo wa kutomtambua mtu anayeitwa Martha
Renju wala Benki ya Standard Chartered ya Hong Kong.
“Sisi msimamo wetu kama IPTL/PAP tunasema
hadharani kwamba hatuitambua Benki ya Standard Chartered ambao hawa kila wakati
wamekuwa wakikimbia mahakama zetu za ndani na kukimbilia nje na hata hukumu hii
ya tuzo ina viashiria vya mabeberu.
“Tuzo husika waliyopewa ni dhahiri
Standard Chartered ni batili kwa mujibu wa sheria. Wao ni kina nani hadi
wakafungie kesi kwa niaba yetu. Hii ni kesi ya ngedere imepelekwa kwa nyani,” alisema
Kutolewa fedha za Escrow
Akizungumzia mchakato wa kutolewa
fedha katika akaunti ya Tegeta Escrow, Makandege alisema mchakato wa kutolewa
kwa fedha hizo ulikuwa wa kihalali kwa mujibu wa sheria za nchi.
Alisema Julai 5, mwaka 2006,
Serikali na IPTL waliingia mkataba wa Escrow ambao ulipelekea kutolewa kwa
fedha hizo kwenye akaunti hiyo iliyokuwa imefunguliwa Benki Kuu ya Tanzania
(BoT) bila kuwahusisha Benki ya Standard Chartered.
“Oktoba 8, 2010 IPTL na Tanesco kwa
kuzingatia kipengele cha 10 cha mkataba huo ambayo kinaeleza kuwa endapo kuna
mgogoro baina ya pande hizo mbili wahusika watakutana na kujadiliana na
hatua ya kuafikiana itahesabika kuisha kwa mgogoro.
“Hata ripoti mbalimbali ikiwemo ya
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) hakuna sehemu yoyote inayoeleza
kuwa zile fedha ni za umma. Hata ICSID imetoa hukumu na kusema si fedha za
Serikali lakini wanakiri zilitolewa kihalali ingawa hawakupewa Standard na kama
kungelikuwa na mgogoro fedha zile singetolewa,” alisema
Kunyang’anywa mitambo
Alipoulizwa kuwa hatua ya suala
hili kugubikwa na utata na utekelezaji wa maazimio manane ya Bunge la 10
likiwemo la wao kunyang’anywa mtambo, Makandege alisema wanajua kuna watu hivi
sasa wanahaingika wakitaka kuona suala hilo linafanyika.
Pamoja na hali hiyo alisema kuwa
mitambo bado ni mali yao kwa mujibu wa sheria na hakuna hatua itakayowafanya
wafanikiwe watu hao ambao hakuwataja.
“Tunajua kuna watu hivi sasa
wanataka kuona suala hili likitekelezwa ikiwemo IPTL kunyang’anywa mtambo,
ninawaambia hakuna jambo kama hilo, nasi kila wakati tumekuwa wazi ikiwemo
kulaani maazimio ya Bunge ambayo ni wazi yalikuwa na lengo la kukimbiza
wawekezaji wazawa. Suala hili hata Rais mstaafu (Jakaya Kikwete) aliliweka wazi
kwa nini lianze sasa baada ya mjadala wake kufungwa,” alisema.
No comments:
Post a Comment