Kamati ya Uongozi ya Chama cha
Wananchi (CUF), imeitisha kikao cha Baraza Kuu la Uongozi Taifa, ili kumhoji
mwenyekiti aliyerudishwa madarakani, Profesa Ibrahim Lipumba.
Wakati wajumbe wa baraza hilo
wakijiandaa kukutana kesho visiwani Zanzibar kutekeleza mpango huo, jana kutwa
nzima, Profesa Lipumba alikuwa na kikao kizito na walinzi wa chama hicho (Blue
Guard) makao makuu ya chama hicho Buguruni, Dar es Salaam.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya
habari jana na Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Zanzibar), Nassor Ahmed Mazrui ilisema
baraza hilo, linamtaka Profesa Lipumba afike mbele ya kikao hicho ili
ajieleze na kujitetea kwanini asichukuliwe hatua za kinidhamu kutokana na
kitendo chake cha kuvamia ofisi za makao makuu na kusababisha uharibifu wa mali.
“Kamati haijakubaliana na maoni na
ushauri uliotolewa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi juu ya
Lipumba. Ilikutana jana (juzi) kwa kikao cha dharura ofisi za Makao
Makuu, Zanzibar na kujadili taarifa ya msajili,” ilisema taarifa
hiyo.
Taarifa hiyo, ilisema kamati
pia ilijadili kitendo cha uvamizi wa ofisi za Buguruni, kilichofanywa na
Profesa Lipumba akiwa na kundi la vijana ambao si wanachama wa CUF.
Alisema baada ya kikao kupitia
maoni ya msajili, kamati iliamua kukataa na kupinga kwa hoja thabiti ushauri na
maoni aliyoyapendekeza na badala yake inaendelea kusimamia maamuzi ya Mkutano
Mkuu Maalumu Taifa uliofanyika Agosti 21, mwaka huu.
“Katika mkutano ule, wajumbe
walikubali Lipumba kujiuzulu kama mwenyekiti wa chama na katika kikao cha
Baraza Kuu la Uongozi Taifa cha Agosti 28, mwaka huu, waliridhia kuwasimamisha
uanachama Lipumba, Magdalena Sakaya, Maftaha Nachuma, Abdul Kambaya, Masoudi
Mhina, Thomas Malima, Ashura Mustafa, Kapasha H. Kapasha, Musa Haji Kombo,
Habibu Mnyaa, Haroub Shamis na kumfukuza uanachama Shashu Lugeye,” alisema.
Taarifa hiyo, ilisema Katiba ya
CUF haina kifungu chochote kinachompa mamlaka Msajili wa Vyama vya Siasa
kupokea rufaa kuhusiana na uamuzi wa vikao vya chama na kubatilisha uamuzi wa
vikao halali.
“Kutokana na kitendo cha kuvamia
ofisi za Buguruni na kusababisha uharibifu wa mali za chama, kamati kwa mujibu
wa ibara ya 85(5) na ibara ya 108 ya Katiba ya CUF ya mwaka 1992 Toleo la mwaka
2014 imeitisha kikao cha Baraza Kuu la Uongozi Taifa Septemba 27, mwaka huu saa
nne asubuhi ofisi za Zanzibar.
“Kwa mujibu wa Ibara ya 12 (6), (7)
na (16) ya Katiba ya CUF ya mwaka 1992 , toleo la mwaka 2014, Kamati imeandaa
ajenda ya kumfikisha Lipumba mbele ya Baraza Kuu na atatakiwa kujieleza na
kujitetea kwa nini baraza lisimchukulie hatua za kinidhamu kwa matendo yake
aliyoyafanya jana (juzi),” alisema.
Katika taarifa hiyo, Mazrui alisema
ibara hizo zinaeleza juu ya kulinda heshima ya chama kwa kuwa na tabia njema,
kutekeleza masharti ya Katiba, kutii kanuni za sheria na sheria ndogondogo za
serikali iliyoundwa kihalali na.
Katika hatua nyingine, Profesa
Lipumba jana kutwa nzima alikuwa na kikao na walinzi wa chama hicho, (Blue
Guard).
Pamoja na mambo mengine, kikao
hicho kilikuwa na ajenda mbili ikiwamo ya kuimarisha ulinzi katika ofisi
zote za chama na kujadili mali za chama ambazo ni pamoja na magari saba na
kompyuta zilizoibwa wakati wa vurugu.
Tamko la Kambaya
Pamoja na hali hiyo jana Naibu
Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano ya Umma, Abdul Kambaya, alitoa tamko
la kuwataka wanachama wa CUF kuwa watulivu kwa ajili ya kukijenga chama hicho.
Alisema pamoja na hali hiyo CUF ni
taasisi na sio eneo la mtu fulani kwani tamko la Naibu Katibu Mkuu CUF
Zanzibar, Nassor Hamed Mazrui la kuukataa ushauri wa Msajili wa Vyama vya Siasa
uliotolewa kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 2002 ni la
upotoshaji.
“Kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya
Siasa ya mwaka 2002, sehemu ya 20, tamko la msajili ni uamuzi na si tu ushauri
kama wanavyotaka kupotosha. Uamuzi huu ni mzito kwa kiwango ambacho hata
mahakama inaweza tu kuurejea lakini si kuufuta (rejea ibara ya 20(2).
“Ieleweke kwamba hii si mara kwanza
msajili kufanya maamuzi kama haya. Mtakumbuka kwamba aliyekuwa Mwenyekiti wetu
Ndugu James Mapalala alienda kwa msajili baada ya kufukuzwa.
“Lakini msajili alitoa uamuzi
kwamba maamuzi yale yalikuwa sahihi Kwa kuwa yalifuata katiba yetu ya CUF. Sasa
iweje hawa wenzetu leo waseme kwamba ule ni ushauri tu?,” alisema na kuhoji
Kambaya ambaye ni mmoja wa wanachama waliosimamishwa na kikao cha Baraza Kuu la
Uongozi.
Alisema kilichofanyika Vuga
Zanzibar ni uasi wa hali ya juu, hivyo watakaa kama chama kutafakari hatua za
kuchukua baada ya kuzuia uasi na kile alichodai mapinduzi haramu kwa chama
hicho.
“Sasa kazi yetu ni kujenga chama.
Wenzetu walioendesha uasi wana hiari ya kujirudi ili tuungane kufanya kazi ya
ujenzi wa chama na kuhudumia wananchi katika maeneo mbalimbali ambapo chama
kimepewa ridhaa ya kuongoza."
No comments:
Post a Comment