
Siku moja baada ya Chama Cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kutangaza kuahirisha kufanya maandamano na
mikutano nchi nzima kupitia oparesheni walioipa jina la UKUTA ( Septemba Mosi)
na kisha kuitaja Oktoba Mosi, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda
nayeye ameitaja siku hiyo kuwa siku maalum ya kupanda miti.
Na ili kufanikisha zoezi hilo,
Jeshi la Wananchi (JWTZ) limeombwa kushiriki huku mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam
akizuia mikutano yoyote ambayo itaonekana haina tija.
Chadema ilikuwa imepanga kuzindua
operesheni iliyoibatiza jina la Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania (Ukuta), kwa
kufanya mikutano na maandamano kote nchini, lakini ikatangaza kuahirisha juzi
ikieleza kuwa imezingatia ushauri kutoka kwa viongozi wa dini, taasisi na watu
mashuhuri.
“Nimezungumza na watu wa hali ya
hewa, wameniambia tukianza mapema miti hii haitakufa. Siku ya Oktoba Mosi kila
mtu atakuwa na mti wake, tutawaarifu kupitia wakuu wa wilaya miti itapatikana
wapi baada ya taratibu zake kukamilika,” alisema Makonda
jana mbele ya Rais Magufuli kwenye mkutano wa 14 wa wahandisi kwenye ukumbi wa
Mlimani City.
Makonda alisema siku hiyo vikosi
vya ulinzi na usalama vitashiriki kupanda miti na kumuomba Rais amsaidie na
amvumilie ili atende kazi yake ya kuhakikisha mkoa wa Dar es Salaam unakuwa na
amani sambamba na kufanikisha kutekeleza mpango huo wa upandaji miti.
Aidha, makonda alipiga marufuku kufanyika kwa mikutano au maandamano yoyote isipokuwa mikutano itakayokuwa inajadili shughuli za maendeleo.
Aidha, makonda alipiga marufuku kufanyika kwa mikutano au maandamano yoyote isipokuwa mikutano itakayokuwa inajadili shughuli za maendeleo.
“Watakaopewa kibali ni wale
wanaojadili maendeleo, lakini si wapigakelele. Mikutano kama hii (ya wahandisi)
inayojadili masuala muhimu kabisa kwa maendeleo ya nchi, itaruhusiwa bila shaka
yoyote.”
Makonda alisema kampeni hiyo
itawahusisha pia wananchi, viongozi wa dini na kamati nzima ya ulinzi na
usalama ya mkoa wa Dar es Salaam na kwamba jumla ya miti milioni 4 inatarajiwa
kupandwa siku hiyo.
Alisema ameamua kushirikisha vyombo
vya ulinzi na usalama kwa sababu ni watiifu na wazalendo kwa Taifa wakati kada
nyingine zimejielekeza kwenye siasa.
Hata hivyo, Rais hakuzungumzia
maombi hayo zaidi ya kusema kuwa Makonda naye amekuwa mhandisi kutokana na
kutoa maelekezo.
Kabla ya Makonda kutangaza Oktoba
Mosi kuwa siku ya kupanda miti, mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema
wamekutana na viongozi wa dini zaidi ya mara moja kwa ajili ya kupata maoni na
ushauri kuhusu maandamano yao, ambayo Jeshi la Polisi liliyapiga marufuku kwa
maelezo kuwa yalikuwa na viashiria vya kuvunja amani.
Baadaye JWTZ ilisema ingeadhimisha
kuzaliwa kwa jeshi hilo kwa askari wake kufanya mazoezi na kuonyesha silaha zao
za angani na nchi kavu, kufanya usafi mitaani na kujitolea damu, huku
likibainisha kuwa linaamini hakungekuwa na maandamano yoyote kwa kuwa
yameshazuiwa.
Katika kuadhimisha miaka 52 ya JWTZ
jana, Makonda alishiriki kufanya usafi na askari hao katika kambi ya Lugalo
iliyopo wilayani Kinondoni.
Makonda aliambatana na kamati ya
amani ya viongozi wa dini wa Dar es Salaam, ikiongozwa na mwenyekiti wake
Alhadi Mussa Salum.
Makonda aliitaja barabara ya Mwenge
–Ubungo kuwa ni miongoni mwa barabara zitakazopandwa miti siku hiyo na
watashirikiana na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads).

No comments:
Post a Comment