
Mfanyabiasha Leonard Materu
(31) amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, akikabiliwa
na mashitaka ya kutuma ujumbe wa kumtishia Rais John Magufuli kupitia mtandao
wa WhatsApp.
Materu ambaye ni mkazi wa Moshi Bar
Kwadiwani, alifikishwa mahakamani hapo jana na kusomewa mashitaka yake na
Wakili wa Serikali, Diana Lukondo mbele ya Hakimu Mkazi Magreth Bankika.
Akisoma mashitaka Wakili Diana
alidai, mshitakiwa huyo amefunguliwa kesi hiyo ya kuchapisha taarifa za uongo
kwenye mtandao wa WhatsApp chini ya Sheria ya Mtandao ya mwaka 2015.
Ilidaiwa kuwa, Julai 17, mwaka huu
jijini Dar es Salaam, Materu aliandika ujumbe wenye lengo la kudanganya umma
kupitia WhatsApp ukisomeka; “Magu ajiandae tunaenda kupindua mpaka
Ikulu.”
Inadaiwa kuwa maneno hayo yalikuwa
na lengo la kumtishia Rais John Magufuli. Baada ya kusomewa mashitaka,
mshitakiwa alikana kutenda kosa hilo, na upande wa Jamhuri ulidai kuwa
upelelezi wa kesi haujakamilika na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa.
Mshitakiwa aliachiwa kwa dhamana
baada ya kutimiza masharti ya dhamana ya kuwa na wadhamini wawili ambao kila
mmoja alisaini hati ya Sh milioni tano. Kesi itatajwa tena Septemba 20, mwaka
huu.

No comments:
Post a Comment