
TAARIFA KWA
VYOMBO VYA HABARI
Mkutano wa 17 wa
Dharura wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kufanyika
Jijini Dar es Salaam
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John
Pombe Magufuli ameitisha Mkutano wa 17 wa Dharura wa Wakuu wa Nchi Wanachama
Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) utakaofanyika Ikulu, Jijini Dar es Salaam
tarehe 09 Septemba, 2016.
Mkutano huo ambao ulitanguliwa na
vikao vya maandalizi vya Makatibu Wakuu na Mawaziri vilivyofanyika Jijini
Arusha utajadili agenda kuu nne ambazo ni:- Mahusiano ya kibiashara na
uwekezaji kati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Umoja wa Ulaya (EU)
kupitia Mkataba wa Ushirikiano wa Kibiashara (EPA).
Agenda zingine ni Kupokea Taarifa
ya Mwezeshaji wa mazungumzo ya Amani nchini Burundi, Mhe. Benjamin William
Mkapa, Rais Mstaafu wa Tanzania; Kupata taarifa ya hatua za kukamilisha
uanachama wa Sudan Kusini kwenye EAC; na Kuapishwa kwa Naibu Katibu Mkuu wa
Jumuiya ya Afrika Mashariki kutoka Rwanda.
Akizungumzia mkutano huo kwa
Waandishi wa Habari, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Mhe. Dkt. Augustine Mahiga amesema kuwa mkutano huu umeitishwa kwa dharura ili
kuzungumzia agenda hizo muhimu hususan ile ya nchi wanachama kukubaliana kwa
pamoja kusaini au kutosaini Mkataba wa EPA ifikapo tarehe 1 Oktoba, 2016.
Kuhusu Mkataba wa EPA, Mhe. Waziri
Mahiga alisema kuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki ilianza mazungumzo na Jumuiya
ya Ulaya ya kushirikiana kibiashara kupitia EPA miaka 14 iliyopita na kuingia
makubaliano ya awali mwaka 2014.
Alieleza kuwa kwa mujibu wa
makubaliano hayo ya awali EU na EAC zilikubaliana Mkataba huo usainiwe kwa
pamoja na nchi zote za Jumuiya mwezi Julai 2016 kabla ya kuanza utekelezaji
wake.
Hata hivyo Tanzania ilitangaza
kutosaini makubaliano hayo kwa sababu mkataba huo unaweza kukwamisha juhudi za
Serikali ya Awamu ya Tano ya kuifanya Tanzania nchi ya Viwanda na Uchumi wa
kati ifikapo 2025.
Aidha, Tanzania inahitaji
kujadiliana zaidi na nchi wanachama ili kujiridhisha kuwa mkataba huo
hautoathiri Mkataba ulioanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki hususan hatua ya
mwanzo ya mkataba ambayo ni Umoja wa Forodha.
Kuhusu nchi nyingine wanachama Mhe.
Mahiga alieleza kwamba, tayari Kenya na Rwanda zimesaini mkataba huo huku
Uganda ikisubiri majadiliano ya nchi wanachama kabla ya kusaini na Burundi
ikijitoa kusaini mkataba huo kwa vile tayari nchi za Ulaya zimeiwekea vikwazo
vya kiuchumi.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya
Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar es Salaam, 07 Septemba 2016.
No comments:
Post a Comment