WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amefanya ziara ya kukagua ujenzi wa makazi mapya ya Waziri Mkuu katika eneo la
Mlimwa na kuagiza umalizike kwa wakati ili aweze kuhamia kama alivyoahidi.
Katika ziara hiyo aliyoifanya jana mchana (Jumatano, Septemba 7, 2016) Waziri Mkuu alisema ameridhishwa na namna kazi ya ujenzi inavyofanyika.
“Nimekuja kukagua makazi mapya na
mahali pa kufanyia kazi. Kazi ya ujenzi inaendelea vizuri, nimejionea mwenyewe
na naamini katika kipindi kifupi watakuwa wamekamilisha,” alisema.
Alisema kutokamilika kwa ujenzi huo
hauwezi kukwamisha azma yake ya kuhamia Dodoma kwa sababu tayari inafahamika
kuwa Makao Makuu ya Ofisi ya Waziri Mkuu yako Dodoma.
Alisema uamuzi wa Serikali kuhamia
Dodoma hautokani na shinikizo la kisiasa bali ni utekelezaji wa Ilani ya Chama
cha Mapinduzi (CCM) ambao chimbuko lake ni agizo lililotolewa Oktoba Mosi, 1973
kwenye Mkutano Mkuu wa 16 wa chama cha TANU.
“Tangu wakati huo Serikali zote
ziliendelea kufanya juhudi mbalimbali za kuandaa miundombinu na hata awamu ya
nne ilisimamia kwa kiwango kikubwa uwekaji wa miundombinu hiyo,” alisema.
“Pia tukumbuke kauli ya Mheshimiwa
Rais aliyotoa kwenye hotuba yake ya Julai 23, 2016 alipochaguliwa kuwa
Mwenyekiti mpya wa CCM, na akairudia tena Julai 25, kwenye maadhimisho ya
kumbukumbu ya Mashujaa na mimi siku hiyo hiyo nikaweka msisitizo,” alisema.
Alisema uamuzi wa Serikali ya awamu
ya tano wa kuhamia Dodoma unakuja baada ya kuridhishwa na ujenzi wa miundombinu
na maeneo ya kutolea huduma za kijamii kwa wageni na wenyeji ikiwemo Hospitali
ya Benjamini Mkapa iliyopo katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) yenye uwezo wa
kutibu magonjwa makubwa kama ya moyo na figo.
Waziri Mkuu alisema tayari Mamlaka
ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA) ina mpango kamambe (master plan) na ina
viwanja vya kutosha kujenga makazi na ofisi mbalimbali.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI
MKUU

No comments:
Post a Comment