Wakati wanasiasa na wasomi
wakimnyooshea kidole Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi (pichani)
kwa uamuzi wake wa kumtambua aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim
Lipumba, mwenyewe ameibuka na kusema kuwa hatua yake hiyo haikulenga kumrudishia
msomi huyo nafasi yake ya uenyekiti.
Jaji Mutungi jana alisema
kuwa alichofanya ni kukishauri chama hicho kuhusu mgogoro uliokuwa ukikisonga na
Lipumba aliamua kutumia ushauri huo kurudi mwenyewe kwenye nafasi yake hiyo
kinyemela.
Kauli hiyo ya Jaji Mutungi imekuja
siku mbili tangu alipotoa waraka unaoelezwa kumtambua Profesa Lipumba kama
kiongozi halali wa CUF licha ya kuandika barua ya kujiuzulu Agosti 6, mwaka
jana akipinga vyama vinavyounda Ukawa kumpa fursa Waziri Mkuu wa zamani, Edward
Lowassa kugombea urais.
“Isome barua yangu…, mimi nimeamua
watu waijadili umenielewa? Ni vizuri wanavyoijadili, ila nilitarajia waijadili
kwa tija sio kwa hasira,”alisema Jaji Mutungi.
Alipoulizwa kuhusu polisi kumsaidia
Profesa Lipumba kuingia katika makao makuu ya CUF kwa mtutu alisema: “Hizo
ni taratibu ambazo (polisi) wanatumia kwa kuzingatia sheria nyingine za nchi.”
Juni mwaka huu, Profesa Lipumba
alimwandikia barua Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad kutengua barua
yake ya kujiuzulu na kutaka arejee kwenye kiti chake, uamuzi uliozusha
mtafaruku huku Mkutano Mkuu wa chama hicho ulioketi Agosti 21 ukiridhia
kujiuzulu kwake licha ya kuwa ulivunjika.
“Barua yangu inajieleza sina haja
ya kuichambua. Nimekujibu baada ya kuona mjadala huo (katika mitandao)
nilitegemea (waliomtukana) wawashauri CUF cha kufanya badala ya kuanza
kunitukana,” alisema Jaji Mutungi.
“Sasa huko mahakamani wanakotaka
kwenda kama mahakama ikiamua kama Mutungi alivyoshauri huko nako watatukana
pia?” alihoji.
Wanasiasa na wasomi
Mwenyekiti wa Chama cha Kijamii
(CCK), Constatine Akitanda alisema alichofanya msajili ni kupandikiza zogo
ndani ya CUF jambo ambalo linasikitisha.
Akitanda alisema ndani ya CUF kuna
bundi ambaye alikuwa anasumbua watu ila msajili ameongezea mgogoro huo na kuwa
alichokifanya si sawa kwa mujibu wa mamlaka yake.
“Unajua hii nchi inachezewa sana
hivi mtu anajiuzulu mwenyewe halafu anaamua kurejea mwenyewe bila kufuata
taratibu ni aibu, lakini nadhani kuna mkono wa mtu,’ alisema.
Mwenyekiti wa Chama cha
ACT-Wazalendo, Anna Mghwira alisema anachokiona ndani ya CUF ni uwepo wa
biashara haramu ambayo inaweza kuua chama hicho.
Alisema ni wakati mwafaka kwa
wafanyabiashara haramu hao wakajulikana katika pande zote kwani ni aibu kuvumilia
kasoro hizo zitawale vyama vya siasa.
Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha
Tanzania Labour (TLP), Dominata Rwechungura alisema migogoro ndani ya vyama vya
siasa ipo, hivyo ni jukumu la CUF kutatua ili kurejesha amani na upendo kati
yao.
Mwenyekiti wa Chama cha United
People Democratic Party (UPDP), Fahimu Dovutwa alisema kinachotokea ni msiba
unaoacha pengo ndani ya CUF na vyama vya siasa nchini.
Dovutwa alisema pia pengo la
mwasisi wa CUF, marehemu Shaban Mloo linaonekana na kuwataka wazee wa chama
hicho kukaa ili kukinusuru chama.
“Huu ni msiba katika siasa za
Tanzania, naomba CUF watafute wazee wao ili waweze kusuluhisha hali hiyo kwa
maslahi ya chama chao kwani pengo la Mloo linaonekana,” alisema.
Katibu wa Habari na Uenezi wa NCCR
Mageuzi, David Kafulila alisema mgogoro wa CUF unaweza kutolewa uamuzi na
mahakama pekee kwa kuwa msajili hana mamlaka ya kufanya alichokifanya. Kafulila
alisema msajili anapaswa kushauri kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa na si
kama alivyoelekeza kwani anaongeza mgogoro zaidi.
Mwenyekiti wa ADC, Hamad Rashid
alishauri CUF kutumia vikao kumaliza tofauti zao, huku akibainisha kuwa ndani
ya chama hicho kuna viashiria vya udikteta na usultani.
Mbunge wa Tandahimba CUF, Katani
Katani alisema kwa sasa wamethibitisha jinsi Lipumba anavyotumika kwani pamoja
na Jeshi la Polisi kukataza maandamano, wafuasi wa Lipumba waliandamana bila
kuzuiwa.
Alisema haiwezekani chama
kikaendeshwa kwa ajenda za watu wachache ambao wanatumikia matumbo yao na
makundi yao na si chama.
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam (UDSM) Kitivo cha Sheria, Dk. Onesmo Kyauke alisema msajili
anakosea na kuwataka CUF wakimbilie mahakamani kupata haki.
No comments:
Post a Comment