Mvutano wa
uenyekiti wa Chama Cha Wananchi (CUF) unatajwa kuwa ni tishio kubwa kwa umoja
wa vyama vya siasa wa Ukawa ambao chama hicho ni sehemu ya nguzo kuu, hali
iliyoibua maoni tofauti kati ya viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema).
Makamu
Mwenyekiti wa Chadema-Bara, Profesa Abdallah Safari, amekiri kuwa mgogoro huo
utaiathiri Ukawa ambayo Profesa Ibrahim Lipumba anayeupigania uenyekiti wa CUF
alikuwa mmoja kati ya waasisi wake lakini aliutosa baadae akipinga uwepo wa
Edward Lowassa.
“Spirit ya
Ukawa ni umoja uliojitokeza baada ya kuaminiwa na Watanzania. Sasa hali hii
inaathiri kwa kiasi fulani,” Alisema Profesa Safari.
Profesa Safari
aliifananisha hali hiyo na kuwa na golikiba mzuri wa timu ya mpira wa miguu
ambaye ni mlemavu wa miguu.
Akizungumzia
barua ya Msajili wa vyama vya siasa iliyoeleza kumtambua Profesa Lipumba kama
mwenyekiti halali wa CUF, Profesa Safari alisema kuwa msajili anajua ukweli
kuwa ushauri wake hauwezi kuchukuliwa kama uamuzi wa mwisho kumrudisha Profesa
Lipumba kwenye nafasi ya uenyekiti wa chama hicho lakini aliamua tu ‘kuvuruga’.
Alisema kuwa
ili kupata uamuzi wenye mamlaka kisheria juu ya mgogoro huo, Profesa Lipumba
anapaswa kwenda Mahakamani na sio CUF.
Hata hivyo,
Mbunge wa Tarime vijijini (Chadema), John Heche alitofautiana na mtazamo wa
Profesa Safari kuhusu mgogoro huo wa CUF akidai kuwa Profesa Lipumba hawezi
kuuyumbisha umoja huo.
“Ukawa haiwezi
kuyumbishwa na Lipumba, Ukawa ilianzishwa na wabunge [wa bunge la katiba]na sio
ushawishi wa Liumba,” alisema Heche.
Juzi, Profesa
Lipumba aliingia kwa nguvu ndani ya ofisi za makao makuu ya CUF zilizoko
Buguruni jijini Dar es Salaam baada ya wafuasi wake kuvunja mlango na kuwapiga
walinzi waliokuwa zamu.
Lipumba
ameendelea kueleza kuwa yeye ndiye mwenyekiti halali wa chama hicho huku
akipinga maamuzi ya kusimamishwa uanachama yaliyotolewa na Baraza Kuu la chama
hicho akidai kikao kilichofikia maamuzi hayo hakikuwa halali.
Kufuatia tukio
la kuvunja ofisi na kuingia ofisini kwa nguvu, Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Nassor
Ahmed Mazrui alisema kuwa wamemuandikia Lipumba barua ya kumtaka ajitetee
mbele ya Baraza Kuu la chama hicho kwanini asichukuliwe hatua kwani kitendo
hicho ni kinyume cha katiba ya chama.
Hata hivyo,
Lipumba amesema hajaipata barua hiyo na wala haitambui.
No comments:
Post a Comment