
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba ameendelea kupingwa ndani ya chama hicho, na safari hii jumuiya ya wanawake wa chama hicho ikiibuka na kumtaka ajiweke kando ili kuepusha mpasuko zaidi.
Aidha, wamewataka wanawake wafuasi
wa chama hicho kote nchini, kuunga mkono uongozi wa muda uliowekwa na Baraza
Kuu la Uongozi wa CUF hivi karibuni, ambao ulimtangaza Julius Mtatiro kuwa
Mwenyekiti wa Kamati ya Muda ya Uongozi ndani ya chama hicho kilichowahi kuwa
kikuu cha upinzani Tanzania.
Akizungumza na waandishi wa habari
bungeni mjini Dodoma jana, Makamu Mwenyekiti wa Taifa wa Jumuiya ya Wanawake wa
CUF, Savelina Mwijage ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalumu, alisema kauli yao
imelenga kuunga mkono hatua iliyochukuliwa na Baraza la Uongozi dhidi ya
wanaotajwa kukiuka Katiba.
Baraza hilo lilikutana Agosti 28,
mwaka huu mjini Zanzibar ikiwa ni hatua ya kukabiliana na hali ya hewa
iliyochafuka baada ya kundi la wanachama kuvamia Mkutano Mkuu Maalumu wa
uchaguzi Agosti 21, mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Mwijage aliyefuatana na wabunge
wengine wanne wa viti maalumu, amesema wanawake ndani ya CUF wamefedheheshwa na
wafuasi wa Profesa Lipumba kwa kufanya vurugu, kudhalilisha wanawake wakati wa
mkutano wa Dar es Salaam na pia kukisababishia chama hasara ya Sh milioni 600
zilitozumika kugharamia mkutano huo.
“Tunalaani kwa nguvu zote vitendo
vya baadhi ya watu wanaotaka kukivuruga chama, lakini pia kuiingiza nchi katika
migogoro ya udini, ukabili, ubara na Uzanzibari. Mbinu hiyo imepitwa na wakati,
tunawaomba Watanzania wote wapuuze siasa hizo za uchochezi,”alisema.
Akizungumza hatua ya kusimamishwa
kwa baadhi ya viongozi 11 wa juu wa chama hicho, wanaodaiwa kushiriki
kukivuruga chama, alisema ni hatua sahihi na kwamba hata Profesa Lipumba
hapaswi kuwa nyuma ya vurugu hizo, kwani aliachia madaraka kwa hiyari yake
wakati chama kikielekea katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.
Kauli ya wanawake hao wa CUF
ilikuja saa chache baada ya Mbunge wa Kaliua, Magdalena Sakaya ambaye ni mbunge
pekee wa kike mwenye jimbo kutoka chama hicho, kuliambia Bunge kuwa hajatikiswa
na uamuzi wa kumsimamisha uanachama na kwamba anaendelea kutimiza majukumu yake
ndani ya chama, ambacho kabla ya mpasuko wa hivi karibuni, ndiye aliyekuwa
Naibu Katibu Mkuu Tanzania Bara.
Mbali ya Lipumba na Sakaya, wengine
waliositishiwa uanachama ni Abdul Kambaya ambaye alikuwa Mkurugenzi wa Habari
na Uenezi wa chama hicho, Ashura Mustapha, Omar Mhina, Thomas Malima, Kapasha
M. Kapasha, Mohamed Habib Mnyaa, Haroub Shamis na Mussa Haji Kombo.
Ashura ni mjumbe wa Baraza Kuu na
aliwahi kuwa Naibu Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano ya Umma CUF wakati Mnyaa
na Kombo, walikuwa wabunge kipindi cha 2010-2015; Mnyaa akiwakilisha Jimbo la
Mkanyageni na Kombo Jimbo la Chake Chake, kisiwani Pemba.
Kutokana na kusimamishwa kwa
viongozi hao, Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui
alimtangaza Mtatiro aliyewahi kuwa Naibu Katibu Mkuu Bara kuwa kiongozi wa
kamati ya uongozi wa muda, inayowajumuisha pia Ahmed Katani na Mwijage ambao ni
wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa.
Katani ni Mbunge wa Tandahimba,
Mtwara wakati Severina alikuwa mjumbe wa kamati kama hiyo ilipoteuliwa Agosti
mwaka jana baada ya Profesa Lipumba kujiuzulu uenyekiti kwa barua ya Agosti 5,
mwaka jana.
Baraza hilo lilimteua pia Joram
Bashange kukaimu nafasi ya Naibu Katibu Mkuu Bara na Mbaraka Maharagande kuwa
Kaimu Naibu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mawasiliano kwa Umma hadi hapo
nafasi hizo zitakapojazwa rasmi kwa mujibu wa masharti ya Katiba ya Chama
hicho.
No comments:
Post a Comment