
Mwenyekiti wa Taasisi
inayoshughulikia masuala ya Afrika (Africa Matters Limited) Mhe. (Baroness)
Lynda Chalker wa Wallasey - Uingereza, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa juhudi kubwa alizozifanya kupiga vita rushwa
na kujenga mazingira bora zaidi kwa uwekezaji.
Mhe. Lynda Chalker ametoa pongezi
hizo jana tarehe 31 Agosti, 2016 Ikulu Jijini Dar es Salaam alipokutana na
kufanya mazungumzo na Rais Magufuli kuhusu masuala mbalimbali ikiwemo hali ya
uwekezaji hapa nchini.
"Mhe Rais amefanya uamuzi
sahihi wa kupiga vita rushwa na kuiweka nchi hii katika njia mpya ya uwekezaji
mzuri na hicho ndicho tumekuwa tukikizungumza, nimejitahidi kutoa ushauri wangu
wa namna mimi na kampuni yangu binafsi tunaweza kumsaidia, nionavyo mambo
yanakwenda katika mwelekeo mzuri" Amesema Mhe. Lynda Chalker.
Kwa Upande wake Rais Magufuli
amemshukuru Mhe. Lynda Chalker kwa ushauri na dhamira yake ya kutaka Tanzania
ipige hatua kimaendeleo na amemuomba kutumia ushawishi wake kuwahamasisha
wawekezaji mbalimbali kutoka nchini Uingereza na kwingineko duniani kuja
kuwekeza nchini Tanzania ili kuharakisha zaidi maendeleo.
Hata hivyo Dkt. Magufuli amesema
wawekezaji wanaokuja Tanzania hawana budi kuwa wawekezaji makini.
"Ninawakaribisha wawekezaji
makini kutoka Uingereza na mahali popote dunia, lakini nisingependa kupata
wawekezaji wababaishaji" Amesisitiza Rais Magufuli.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi
wa Mawasiliano, IKULU
Dar es Salaam
31 Agosti, 2016

No comments:
Post a Comment