Rais Dkt John Magufuli, amewaomba radhi wananchi 644 waliokuwa wakiishi
Kota za Magomeni jijini Dar es Salaam, na kuwaahidi atakamilisha ujenzi wa
nyumba zao katika kipindi cha mwaka mmoja.
Pia aliwaahidi wananchi hao kuwa watakuwa wakiishi bure
kwa miaka mitano kabla ya kuuziwa nyumba hizo kwa bei ya chini kwa kufidia
mateso waliyoyapata kwa zaidi ya miaka minne baada ya kuondolewa katika eneo
hilo.
Akizungumza na wananchi hao, Rais alisema serikali
ilichukua eneo lenye hekali 33 na ujenzi wa nyumba hizo utakaoanza katika muda
wa miezi miwili kuanzia sasa na utakapokamilika kipaumbele kitapewa kwa wakazi
waliokuwa wakiishi katika eneo hilo.
Kwa upande wake waziri wa ardhi, nyumba, maendeleo na
makazi, William Lukuvi, alisema serikali tayari imezichukua nyumba zaidi ya
5000 katika mikoa ishirini zinazomilikiwa na shirika la nyumba la taifa ili
kuepuka uwezekano wa kutapeliwa kama ilivyofanyika katika nyumba za Magomeni
Kota.
Baadhi ya wananchi waliokuwa wakiishi katika nyumba hizo
, wameipongeza serikali kwa jitihada zake za kuwatetea wanyonge na kwamba
uamuzi huo wa Rais ni habari njema kwao.
Katika hatua nyingine, Rais Magufuli ametoa siku 7 kwa
taasisi zilizopanga kwenye nyumba za NHC kulipa madeni yao.
“Nimetoa siku 7 kwa taasisi zote za serikali zinazodaiwa
na shirika la nyumba la taifa kulipa madeni hayo kwa mkurugenzi mkuu wa shirika
hilo, uziondee taasisi zote za serikali ndani ya majengo yake kama zitashindwa
kulipa katika kipindi cha juma moja,” aliagiza.
BY: EMMY MWAIPOPO
No comments:
Post a Comment