
Mamlaka ya Maabara ya Mkemia
Mkuu wa Serikali itakuwa na uwezo na mamlaka ya kuchunguza watu waliozaliwa na
jinsi mbili na kubaini jinsi tawala yenye nguvu zaidi.
Muswada wa Sheria ya Mamlaka ya
Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali wa Mwaka 2016, uliopitishwa juzi usiku saa
nne bungeni unampa Mkemia Mkuu mamlaka ya kuchunguza na kubaini jinsi ya mtu na
kutatua utata kwa mtu atakayekuwa amezaliwa na jinsi mbili.
“Waheshimiwa wabunge naona wengi
wenu mnadhani mkemia mkuu kazi yake ni kuchunguza vinasaba kubaini uhalali wa
mzazi na mtoto, maana naona wabunge wengi wamelishabikia hilo, lakini katika
teknolojia ya vinasaba yanahusu pia utambuzi wa jinsi, watu unakuta wanawake au
wanaume wanazaliwa jinsi ya kike na kiume, kwa hiyo tunaangalia jinsi tawala ni
ipi ina nguvu,” alisema Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee
na Watoto, Ummy Mwalimu.
Ummy alikuwa akijibu michango ya
wabunge waliochangia wakati wa kujadili Muswada wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia
Mkuu 2016 kabla ya kuupitisha juzi usiku, waliotaka mamlaka ya maabara ya
mkemia mkuu kutoa elimu kwa wananchi juu ya shughuli zake.
Alisema kwa sheria hiyo, sasa
mkemia mkuu kupitia maabara yake anaweza kusema jinsi ya kike au ya kiume ndio
yenye nguvu, lakini pia kuna suala la kuhakikisha utambuzi wa mwanadamu hasa
wakati yanapotokea majanga pamoja na watu wanaosafiri kwa makundi.
Alikubaliana na wabunge kuwa iko
haja ya kuwaelimisha wananchi juu ya kazi za maabara ya mkemia mkuu ambao wengi
wao wanadhani inafanya kazi hiyo tu ya kubaini vinasaba vya mzazi na mtoto,
lakini sasa wafahamu hata waliozaliwa na jinsi mbili wanaweza kutegua utata huo
kwa kubaini jinsi tawala au jinsi yenye nguvu zaidi kama ni ya kiume au ya
kike.
Alisema Maabara ya Mkemia Mkuu wa
Serikali imekuwepo kihistoria tangu mwaka 1890 na imekuwa chombo cha kiserikali
cha uchunguzi cha kikemia wa kimaabara kwa bidhaa mbalimbali na kuongeza kuwa
imekuwa ikifanya uchunguzi wa kikemia wa vyakula, dawa na vipodozi hasa pale
inapotokea utata au kuhusisha masuala ya kesi za jinai.
Akifafanua zaidi, alisema kwa
upande wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) wao wanafanya udhibiti wa ubora wa
chakula, dawa na vipodozi na maabara hii inafanya uchunguzi wa kikemia.
“Maabara ya Mkemia Mkuu kazi yake
ni kufanya uchunguzi wa kikemia, vinasaba, kesi za jinai na sayansi jinai.
Chombo hiki hakipimi kudhibiti ila kufanya uchunguzi kwa ajili ya vitu vyenye
maslahi ya taifa au masuala yenye utatanishi na ushindanishi,” alisema waziri
huyo.
Akitoa mfano wa mahindi, alisema
kulikuwa na tatizo la sumu kuvu, kwa hiyo mkemia mkuu anafanya uchunguzi wa
kimaabara na kusema wamekuta mahindi yana sumu au la, au anaweza mfanyabiashara
kuleta maziwa ya mtoto TFDA ikapata mashaka, mkemia mkuu atayafanya uchunguzi
wa maabara atasema kama kuna sumu ama kuna kemikali isiyo salama kwa matumizi
wa binadamu.
“Baada ya uchunguzi wa kimaabara
mwenye jukumu la kusema mahindi haya yasiuzwe au maziwa haya yasiuzwe ni TFDA
na sio maabara ya mkemia mkuu. Vile mfanyabiashara anaweza kuleta bidhaa, TFDA
ikaitilia mashaka, kwa hiyo huyu mwenye bidhaa anaweza kukata rufaa kwa mkemia
mkuu ili apimiwe bidhaa yake kuithibitishia TFDA kuwa bidhaa yake ni salama,” alisema.
Waziri Ummy alikuwa akijibu hoja za
wabunge, ambao walikuwa wana hofu kuwa Maabara ya Mkemia Mkuu inaweza kuingilia
kazi za taasisi kama TFDA na Shirika la Viwango Tanzania (TBS).
Alizungumzia pia kuhusu kuipa
mamlaka ya mwisho maabara hiyo, akisema katika nchi zote duniani zenye maabara
hizo, lazima serikali iwe na msemaji wa mwisho wa uchunguzi wa masuala ya
kimaabara na kikemia, vinasaba, sayansi jinai na kesi za jinai, lakini pia
haifuti sheria wala maabara zingine za uchunguzi zilizoanzishwa kwa mujibu wa
sheria mbalimbali.
Kuhusu kutenga bajeti ya kutosha,
Ummy alisema serikali imepokea maoni ya wabunge na kuwa baada ya kupitisha
muswada huo maabara hiyo imepewa hadhi ya mamlaka na sasa imepewa hadhi na
hivyo fungu lake lazima liwe zuri kwa ajili kuendesha shughuli za maabara
lakini pia kuajiri watumishi 400 kwani waliopo sasa 192 hawatoshi.
Waziri Ummy alisema wamepokea
ushauri wa Kamati ya Kudumu ya Bunge, kufanya uchunguzi wa matumizi ya shisha
na kuongeza kuwa tayari mkemia mkuu alifanya uchunguzi na kubaini watumiaji wa
shisha wanachanganya bangi, heroine na kokeni na ndio maana serikali ilipiga
marufuku kuitumia.
Hata hivyo, alisema sasa itajikita
zaidi kuchunguza ili kubaini viambata kiasi gani vilivyopo katika shisha na kwa
nini serikali iendelee kupiga marufuku matumizi ya shisha nchini.
No comments:
Post a Comment