
Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya Jumamosi alikanusha ripoti za vyombo vya habari kwamba kuna mvutano baina ya Kenya na Tanzania.
Akizungumza mjini Mombasa wakati wa
ufunguzi gati la makontena katika bandari ya Mombasa, Kenyatta alipuuzia maneno
kwamba kuna mvutano wowote na badala yake akasema kuwa nchi hizo zinasaidiana.
Alisema anaona kwenye vyombo vya
habari kwamba kuna “mgogoro baina yetu, lakini nataka kusema wazi wazi kwamba
Kenya na Tanzania hazina mgogoro wowote baina yao,” alisema.
Kenyatta alisema uchumi wa nchi
hizo mbili umefungana kwa miaka mingi na ni kwa ajili ya faida ya watu wa nchi
hizo mbili.
Alitaja kufunguliwa kwa njia
inayojulikana kama “northern frontier” ambayo itaunganisha bandari ya Mombasa
kupitia mkoa wa Kilimanjaro, Tanzania, hadi Bujumbura, Burundi – njia ambayo
itafupisha urefu wa kutoka Bujumbura hadi Mombasa kwa kilomita 300 nzima.
“Afrika Mashariki haiko katika
mashindano ya wenyewe kwa wenyewe,” alisema Kenyatta. “Afrika Mashariki
inashindana na dunia. Tunataka kujaliana (pale penye mapungufu). Tunataka
tutumie nguvu zetu ili kukua, kuendeleza na kuinua uchumi wetu,” alisema.
Kutokuwepo kwa Rais John Magufuli
wa Tanzania katika mkutano wa hivi karibuni wa kimataifa na Tokyo mjini Nairobi
kulizusha uvumi kuhusu uhusiano wa nchi za eneo hilo.
Kiongozi huyo wa Tanzania
ametembelea Uganda na Rwanda tu tangu achukue madaraka Oktoba mwaka jana ukilinganisha
na rais aliyemtangulia Jakaya Kikwete ambaye alikuwa akisafiri sana nchi za
nje.
Rais Magufuli pia hakuhudhuria
mikutano karibu mitano ya kimataifa, ikiwa ni pamoja na mkutano wa shirika la
biashara duniani na mikutano mikuu ya AU mjini Addis Ababa na ule wa Kigali
Rwanda hivi karibuni.
No comments:
Post a Comment