
Umoja wa Vijana wa Chama cha
Mapinduzi (UVCCM), umewavaa viongozi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema) kwa kile walichodai kuendesha siasa za maigizo baada ya kushindwa
kuzindua Operesheni UKUTA, Septemba 1.
Kupitia taaria yake kwa vyombo vya
habari, Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka, amesema kuwa Chadema
walijua kuwa hawana ubavu wa kufanya maandamano na mikutano nchi nzima Septemba
1 na kwamba walichofanya ni kuwatia hofu wananchi.
“UVCCM tulijua, tulielewa na
kutambua bayana kwamba Chadema walikuwa wanafanya maigizo katika siasa, hawana
ubavu wala jeuri ya kuandamana kwa madai ya kipuuzi na ambayo sio ya msingi kwa
mustakabali wa nchi yetu,” alisema Shaka.
Aidha, Shaka alikanusha sababu
zilizotolewa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kuahirisha maandamano hayo
kuwa wameombwa na viongozi wa dini ili waweze kukaa na pande zote kujaribu
kutafuta suluhu kwa amani.
“UVCCM inatamka bayana kuwa hakuna
majadiliano, mazungumzo wala mijadala itakayojadiliwa kati ya Serikali ya CCM
na Chadema. Tunaomba Serikali ya Rais John Magufuli iendelee na mikakati yake
ya kisera,” Shaka ameongeza.
Kaimu Katibu Mkuu huyo wa UVCCM alisisitiza
kuwa Chadema hawana ubavu wa kufanya maandamano na mikuano nchi nzima Oktoba 1
kama walivyosema, baada ya kushindwa kufanya hivyo Septemba 1.
Shaka amesema wanachokifanya hivi
sasa Chadema kinatokana na kushindwa kubuni mikakati ya kufanya siasa ili chama
chao kiimarike na kukubarika.
Juzi, Chadema walitangaza
kuahirisha uzinduzi wa oparesheni UKUTA nchi nzima, iliyokuwa imepangwa
kufanyika jana (Septemba 1) kwa maandamano na mikutano nchi nzima.
UVCCM pia walitangaza kuahirisha
maandamano yao ya nchi nzima waliyokuwa wamepanga kuyafanya Agosti 31 kwa lengo
la kumpongeza Rais Magufuli kwa kazi aliyoifanya ndani ya kipindi kifupi.
Maandamano ya pande zote mbili
yalipigwa marufuku na Jeshi la Polisi nchini.

No comments:
Post a Comment