
Kambi rasmi ya upinzani imepanga
kufanya vikao vya kujadili suluhu ya kudumu ya mgogoro na Naibu Spika, Dk Tulia
Ackson uliosababisha wabunge wanaounda Ukawa kususia vikao vinavyoendeshwa na
kiongozi huyo.
Vikao hivyo vinapangwa kufanyika wakati mkutano wa nne ukianza rasmi kesho, baada ya kuahirishwa mwishoni mwa Juni mwaka huu wakati wa mkutano wa Bajeti.
Mbunge wa Vunjo (NCCR- Mageuzi),
James Mbatia alieleza jana kuwa uamuzi wa kufanya vikao hivyo umefikiwa baada
ya upinzani kukaa kikao na viongozi wa dini Agosti 24 mwaka huu ili kutafuta
suluhu ya kudumu.
“Kikao cha kwanza tutakaa kamati ya
uongozi ya wabunge wa upinzani kujadili suala hilo na baadaye tutamaliza na
kikao cha wabunge wote ili kubaini njia endelevu za kumaliza jambo hilo,” alisema Mbatia
ambaye ni Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi.
Wabunge wa Ukawa wamekuwa wakisusia
vikao vinavyoendeshwa na Naibu Spika kwa madai ya kutoridhishwa na uongozi wake
tangu Mei mwaka huu, baada ya Dk Tulia kukataa kujadili hoja ya kufukuzwa
wanafunzi zaidi ya 8,000 stashahada ya ualimu wa Chuo Kikuu cha Dodoma
(Udom).
Hata wakati wakisubiri kufanyika
vikao hivyo ambavyo Mbatia hakutaka kuelezea kwa undani, upinzani ulitangaza
kurudi bungeni baada ya mkutano wao na viongozi wa dini.
Katika mkutano na wanahabari Agosti
25, Mbatia kwa niaba ya vyama vilivyoshiriki mkutano huo wakiwamo
ACT-Wazalendo, alisema wangejadiliana namna ya kufanikisha jambo hilo kama
sehemu ya kutii ushauri wa viongozi hao wa kiroho.
Hata hivyo, haijawekwa bayana iwapo
kesho Ukawa wataendelea na vikao hata kama Dk Tulia ataendelea kuongoza kiti
hicho ama la.
Mbatia alisema jana kuwa watatoa taarifa rasmi leo namna vikao hivyo vitakavyofanyika na siku husika.
Mbatia alisema jana kuwa watatoa taarifa rasmi leo namna vikao hivyo vitakavyofanyika na siku husika.
Kuhusu kupata taarifa ya mwenendo
wa mchakato wa kutafuta maridhiano ulioelezwa na Spika Job Ndugai hivi
karibuni, Mbatia alisema hawajapata chochote na wao wanasikia kwenye vyombo vya
habari kama wengine.
Alipoulizwa ni lini vikao vya
maridhiano kati ya pande hizo yataanza, Ofisa Habari, Elimu na Mawasiliano wa
Bunge, Owen Mwandumbya alisema Spika anatarajiwa kufika ofisini leo na kwamba
kama ataona kuna haja ya kufanya hivyo atapanga utaratibu wa namna anavyoona
inafaa.

No comments:
Post a Comment