Waziri wa nchi, Ofisi ya Waziri
Mkuu, Sera, Uratibu, Bunge, Vijana na Watu Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama
ametoa siku saba kwa taasisi za serikali, wizara, kampuni na watu binafsi
kuhakikisha wanalipa madeni wanayodaiwa na Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii
(NSSF).
Waziri Mhagama pia ameziagiza bodi za wadhamini za mifuko mingine ya hifadhi ya jamii, kuhakikisha zinawashinikiza wadeni wao kulipa madeni yote wanayodaiwa ili kuiwezesha mifuko hiyo kujiendesha kwa ufanisi zaidi.
Ametoa tamko hilo mwishoni mwa wiki
jijini Dar es Salaam, alipotembelea miradi ya nyumba za NSSF iliyopo wilayani
Kigamboni mkoani Dar es Salaam.
Amemtaka Katibu Mkuu wa wizara
hiyo, Erick Shitindi kuhakikisha uongozi wa mifuko unampatia ripoti ya hatua
zilizochukuliwa dhidi ya wahusika wote walioshindwa kulipa madeni yao kwa
mifuko yao.
“Ninafahamu fika kuna mikataba
ambayo ilisainiwa na pande zote mbili kabla ya kutolewa kwa hiyo mikopo na
makubaliano mengine hivyo naomba basi mikataba hiyo itumike kufanikisha agizo
hili,’’ alisema.
Pia alimuagiza Mwenyekiti wa Bodi
ya Wadhamini wa NSSF, Profesa Samwel Wangwe kuhakikisha anampatia ripoti
muafaka ya utekelezaji wa agizo hilo.
“Kwa niaba ya serikali, ninataka
kuona kwamba wadaiwa wote wa mifuko hii bila kujali nafasi zao kiuchumi au
kisiasa wanalipa madeni wanayodaiwa…hii lazima ijumuishe kampuni, wawekezaji na
taasisi za serikali,’’ alisisitiza.
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF,
Profesa Godius Kahyarara alisema licha ya mfuko wake kufanikisha utekelezaji wa
miradi mbalimbali ikiwemo majengo, bado wateja wake wengi hawajalipa madeni
wanayodaiwa na mfuko huo ikiwemo watu binafsi, taasisi za serikali na binafsi
wakiwemo pia wale walionunua nyumba za shirika hilo.
Alisema shirika hilo, bado linadai
Sh bilioni 20 kutoka kwa wapangaji wake, deni linalohusisha pia dola za
Marekani milioni 1.2.
Alifafanua kuwa kiasi kingine cha
Sh bilioni 86, kinadaiwa kama adhabu kutoka kwa waajiri walioshindwa
kukamilisha makato ya wafanyakazi wao.
Madeni mengine ni pamoja na deni la
Sh milioni 42 na dola za Marekani milioni 35.9 zilizotolewa kama mikopo kwa
sekta binafsi mbalimbali huku mkopo mwingine wa Sh bilioni 38 ulitolewa kupitia
Saccs na bado hazijarejeshwa.
“Hata hivyo, tumeanza kuchukua hatua
mahsusi kulingana na matakwa ya sheria kuhakikisha kwamba madeni yote
yanalipwa,’’ alibainisha Profesa Kahyarara.
Waziri nchi ofisi ya waziri mkuu sera, uratibu, bunge ,vijana na watu wenye ulemavu Mhe. Jenister Mhagama akiwa ameambatana na uongozi wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) alipotembelea miradi ya nyumba za NSSF iliyopo wilayani Kigamboni mwishoni mwa wiki.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa NSSF Prof Samwel Wangwe. (kushoto) akizungumza mbele ya Waziri nchi ofisi ya waziri mkuu sera, uratibu, bunge ,vijana na watu wenye ulemavu Mhe. Jenister Mhagama wakati waziri huyo alipotembelea miradi ya nyumba za NSSF iliyopo wilayani Kigamboni mwishoni mwa wiki. Wengine ni pamoja na Mkurugenzi mkuu wa NSSF, Profesa Godius Kahyarara (kulia).
Mkurugenzi mkuu wa NSSF, Profesa Godius Kahyarara (kulia) akizungumza mbele ya Waziri nchi ofisi ya waziri mkuu sera, uratibu, bunge ,vijana na watu wenye ulemavu Mhe. Jenister Mhagama wakati waziri huyo alipotembelea miradi ya nyumba za NSSF iliyopo wilayani Kigamboni mwishoni mwa wiki. Wengine ni pamoja na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa NSSF Prof Samwel Wangwe (kushoto).
No comments:
Post a Comment