
Na: Lilian Lundo- Maelezo
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Dkt. Hussein Ali
Mwinyi amewahakikishia watanzania kwamba mipaka ya Tanzania ni salama.
Mhe. Dkt. Mwinyi ameyasema hayo katika kipindi cha Tunatekeleza
kinachorushwa na Televisheni ya Taifa (TBC) alipokuwa akieleza mikakati ya
wizara hiyo katika kuhakikisha mipaka ya Tanzania iko salama.
“Nchi iko salama, mipaka ya nchi iko shwari, ziko changamoto
chache za nchi zinazotuzunguka kuwepo katika machafuko mfano Burundi hivyo
wananchi wake kukimbilia Tanzania,” alifafanua Mhe. Dkt. Mwinyi.
Amesema Tanzania sio kisiwa, imejiunga na jumuiya mbali mbali
kama Jumuiya ya Afrika Mashariki, Jumuiya ya Umoja wa Afrika na Jumuiya ya
Umoja wa Mataifa hivyo kupitia Jumuiya hizo Tanzania hupata maelekezo ya
kuwapokea wakimbizi kutoka nchi zenye machafuko.
Hata hivyo Mhe. Dkt. Mwinyi amesema kuwa Wizara yake kwa
kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi inahakikisha wakimbizi
wanaoingia nchini wanafuata utaratibu unaotakiwa bila kuvunja sheria za nchi.
Pia ameeleza kuwa Tanzania inaendelea na mazungumzo ya amani na
nchi ya Malawi juu ya mgogoro wa umiliki wa Ziwa Nyasa baina ya nchi hizo mbili
ili kupata ufumbuzi wa amani, ambapo mazungumzo hayo ya yanaongozwa na Rais
Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Benjamin William Mkapa.
Aidha, Mhe. Dkt. Mwinyi amesema kuwa kutokana na Wizara hiyo
kufanya vizuri katika Ulinzi na Amani ya Nchi, Jumuiya ya Umoja wa Afrika na
Jumuiya ya Umoja wa Mataifa imeiomba nchi ya Tanzania kutoa Ulinzi wa
Amani kwa nchi za Sudani, Kongo na Lebanoni kutokana na machuko yanayoendelea
katika nchi hizo.
Vile vile ameeleza kuwa, ushiriki wa Jeshi la Tanzania katika
nchi zenye machafuko kunaisaidia Jeshi hilo kupata mafunzo ya kivita kutokana
na Tanzania kuwa ni nchi ya amani hivyo kufanya baadhi ya wanajeshi kutoshiriki
mafunzo ya uhalisia ya kivita tangu wanapoajiriwa mpaka kustaafu.

No comments:
Post a Comment