
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu
imewasomea maelezo ya awali (PH) washtakiwa wanane wakiwamo, wabunge watatu wa
Chama cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema) katika kesi ya kumpiga na kumjeruhi
Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam(RAS),Theresia Mmbando.
Akisoma maelezo hayo mbele ya
Hakimu, Huruma Shaidi, Wakili wa Jamhuri, Frola Massawe aliwataja washtakiwa
hao kuwa ni pamoja na Halima Mdee (Kawe), Mwita Waitara (Ukonga), Saed Kubenea
(Ubungo), aliyekuwa Diwani wa Kata ya Saranga, Ephreim Kinyafu, Diwani wa Kata
ya Kimanga, Manase Njema na mfanyabiashara Rafii Juma.
Wakili Massawe alidai mahakamani
hapo kuwa, washtakiwa hao kwa pamoja wanadaiwa kutenda kosa hilo Februari 27,
mwaka huu katika ukumbi wa Karimjee, ulioko wilayani Ilala, jijini Dar es
Salaam ambako kulikuwa na uchaguzi wa meya na msadizi wake.
Alidai kuwa,katika ukumbi
huo,kulitolewa taarifa ya kutokuwepo kwa uchaguzi huo kutokana na kuwepo kwa
zuio kutoka Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ambapo liliwataka kutofanya
uchaguzi huo mpaka zuio hilo litakapomalizika ndipo uchaguzi ufanyike.
Alidai kuwa, mshtakiwa wa kwanza
ambaye si mbunge (Rafii Juma), hakuridhishwa na taarifa hiyo ndipo
aliposhirikiana na washtakiwa wengine kwa kumvamia, kumpiga na kumchania nguo
RAS Mmbando hali iliyosababishia majeraha.
Alidai, baada ya kutokea kwa vurugu
hizo, polisi waliingilia kati na kumuuliza kama aliweza kuwafahamu waliompiga,
baada ya kuulizwa hivyo, alidai kumfahamu mshtakiwa wa pili, ambaye ni Halima
Mdee.
Alidai kuwa, baada ya hapo, polisi
walilazimika kuchukua daftari la mahudhurio ya siku hiyo na kuanza kuita majina
mmoja baada ya mwingine na kupiga gwaride la utambulisho ambalo lilimsaidia
kuwatambua washtakiwa wote na kukamatwa na kuwafikisha polisi na mahakamani.
Baada ya kusomewa maelezo hayo,
washtakiwa hao walikubali taarifa zao binafsi lakini walikana shtaka
linalowakabili.
Hata hivyo, upande wa mashtaka
ulidai kuleta mashaidi 16 ambao watatoa ushaidi kwenye kesi hiyo.
Kutokana na hali hiyo, Hakimu
Shaidi alihairisha kesi hiyo hadi Novemba 14 mwaka huu kwa ajili ya kuanza
kusikiliza ushaidi.

No comments:
Post a Comment