YAH: MSIMAMO NA USHAURI WA MSAJILI
WA VYAMA VYA SIASA KUHUSU UONGOZI WA KITAIFA WA CHAMA CHA THE CIVIC UNITED
FRONT (CUF)
Tafadhali husika na somo hapo juu
pamoja na barua yako ya tarehe 23 Septemba 2016 yenye Kumb Na. HA.322/362/14/85
kuhusu somo tajwa.
Baraza Kuu la Uongozi la The Civic
United Front (CUF) – Chama Cha Wananchi, kupitia Ofisi ya Katibu Mkuu wa Chama,
limepokea barua yako tajwa hapo juu pamoja na taarifa fupi inayoainisha msimamo
na ushauri wa Msajili wa Vyama vya Siasa kwa Chama cha The Civic United Front
(CUF) na kuijadili kwa kina. Yafuatayo ni majibu na msimamo wa Baraza Kuu la
Uongozi la Taifa la CUF ambayo tunapenda kuyawasilisha ili ofisi yako iyafanyie
kazi.
Awali ya yote, tunakupongeza kwa
namna ulivyofuatilia kwa kina, kupitia wadhifa wako kama Msajili wa Vyama Vya
Siasa Tanzania, malalamiko yaliyowasilishwa kwako na watu uliowatambua kwenye
taarifa yako fupi.
Aidha, tumebaini kuwa ofisi yako
imejikita katika kutoa tafsiri ya Katiba ya Chama cha The Civic United Front
(CUF) toleo la mwaka 2014 pamoja na tafsiri ya matukio na maamuzi ya vikao vya
Chama kwa mujibu wa ufahamu wako.
Pili, tumebaini kuwa ofisi ya Msajili
wa Vyama vya siasa haina mamlaka ya kisheria kutoa “Msimamo na Muongozo” kwa
chama cha siasa kilichosajiliwa nchini Tanzania.
Majukumu ya ofisi yako kwa mujibu
wa sheria iliyoanzisha ofisi yako, Sheria ya Vyama Vya Siasa Sura ya 258,
haikupi mamlaka ya kutoa msimamo na Muongozo.
Badala yake, unapewa mamlaka ya
kuhifadhi kumbukumbu na taarifa za vyama vya siasa. Majibu haya yanatokana na
ukweli kuwa ofisi yako imewahi kuonywa na Mahakama Kuu ya Tanzania, Dar es
Salaam katika shauri la Madai Na. 6 la mwaka 2003 baina ya Emmanuel Nyenyemela
and Another Versus Registrar of Political Parties and Others mbele ya
Mheshimiwa Jaji Mihayo. Mahakama ilieleza kama ifuatavyo kwenye ukurasa wa pili
wa hukumu:
“In the same vein, I do not see
anywhere in the Political Parties Act where the Registrar has power to bless or
condemn meetings of political parties or decisions that they make”. (Katika
Muktadha huo huo sioni mahali popote kwenye Sheria ya Vyama vya Siasa ambapo
Msajili wa Vyama ana mamlaka ya kubariki au kupinga vikao vya vyama vya suasa
au maamuzi yanayofanywa na vikao hivyo).
Tunapenda utambue kuwa uamuzi na
muongozo huo wa Mahakama Kuu ya Tanzania haukuwahi kutenguliwa na Mahakama
yoyote ile na hivyo tunaamini wewe ukiwa na weledi katika taaluma ya sheria na
Jaji wa Mahakama kuu, unafahamu uamuzi huo na namna ya kuutumia.
Tatu, pamoja na kubaini yaliyomo
kwenye aya zilizotangulia hapo juu, tunapenda upokee majibu yetu kuhusiana na
kila kipengele ulichoongelea kwenye Taarifa yako fupi kama ifuatavyo:
1. MAMLAKA NA WAJIBU WA MSAJILI
KUSHUGHULIKIA MGOGORO HUU
Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la
The Civic United Front CUF linasikitika na upotoshaji wa makusudi uliofanywa na
ofisi yako kuhusu tafsiri ya vifungu vya Sheria ya Vyama Vya siasa, Sura ya 258
ulivyovitaja katika ukurasa wa pili wa Taarifa yako fupi ili kujipa mamlaka ya
kushughulikia kile ulichokiita mgogoro wa Uongozi katika Chama chetu.
Tunapenda urejee vifungu
ulivyotumia ambavyo tunavichapisha tena hapa chini:
Kifungu cha “8A (1) There shall be
a Registrar of Political Parties into which names, addresses, and other
particulars of Registered Political Parties or national leaders of Political
Parties shall be entered.” (Kutakuwa na Msajili wa Vyama vya Siasa ambako
majina, anwani na taarifa zingine za Vyama vya Siasa vilivyosajiliwa au
viongozi wa kitaifa wa vyama vya siasa zitawekwa).
Kifungu cha 10(f) “No Political
Party shall be qualified to be fully registered unless …..(a)…….(e) (Hakuna
Chama cha siasa kitakachofaulu kupewa usajili wa kudumu hadi……)
(f) it has submitted the names of
the national leadership of the party and such leadership draws its members from
both Tanzania Zanzibar and Mainland Tanzania, and” (kiwe kimewasilisha majina
ya uongozi wa kitaifa na uongozi wa chama hicho uundwe na wanachama kutoka
Tanzania Zanzibar na Tanzania Bara, na)
Ukivisoma vifungu hivyo hapo juu,
katika sheria tajwa, utabaini kuwa havina kabisa uhusiano na kukupa wewe
mamlaka au wajibu wa kuchunguza na kujiridhisha kuhusu usahihi wa mabadiliko
katika uongozi wa Kitaifa wa Chama na ama kutengua au kubariki maamuzi halali
ya vikao halali vya chama chochote. Zingatia pia hukumu ya Mahakama Kuu ya
Tanzania ambayo tayari tumeitaja hapo juu. Tumejiridhisha kuwa mamlaka uliyojitwisha
hayakuwa yako na pia hukuyatenda kwa kuzingatia misingi ya haki.
2. KUJIUZULU KWA PROFESA IBRAHIM
LIPUMBA NA KUTENGUA BARUA YAKE YA KUJIUZULU
Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la
The Civic United Front CUF linatambua kuwa Chama cha The Civic United Front
(CUF) kinaongozwa na Katiba yake halali, toleo la mwaka 2014. Tunapenda utambue
kuwa kujiuzulu kwa kiongozi ni wakati wowote kwa mujibu wa Ibara ya 117(1).
Kuhusu utaratibu uliowekwa na ibara ya 117(2) hauathiri haki ya kiongozi
kujiuzulu wakati wowote.
Prof. Ibrahim Haruna Lipumba
aliandika barua ya kujiuzulu nafasi ya Mwenyekiti wa CUF Taifa kuanzia tarehe
5/08/2015 ambayo ni siku aliyoandika barua hiyo na aliutangaza uamuzi wake huo
mbele ya vyombo vya habari tarehe 6/8/2015.
Katika Barua yake ya kung’atuka
wadhifa wa Mwenyekiti wa Taifa wa CUF ilisema ;
”Leo tarehe 5 Agosti 2015 najiuzulu
rasmi nafasi ya Mwenyekiti wa Taifa wa CUF. Naendelea kuwa Mwanachama na kadi
yangu nimeilipia mpaka 2020.”
Prof. Lipumba alitekeleza kujiuzulu
kwake bila kusubiri kukubaliwa na Mkutano Mkuu wa Chama kwa mujibu wa Ibara
117(2) ya Katiba ya Chama. Prof. Lipumba alikua na mamlaka ya kuhakikisha kuwa
Mkutano Mkuu unaitishwa ili kukubali kujiuzulu kwake lakini hakufanya hivyo.
Kama ulivyoeleza katika taarifa
yako, Katiba ya CUF inatambua haki ya kujiuzulu uongozi lakini haizungumzii
kutengua uamuzi wa kujiuzulu. Prof Lipumba asingeweza kutengua uamuzi wake wa
kujiuzulu kwa sababu alishautekeleza. Na aliacha ofisi na majukumu ya
Mwenyekiti wa Taifa wa CUF kwa mujibu wa Ibara ya 91 ya Katiba ya Chama kwa
zaidi ya miezi kumi. Kuna msemo “you can not eat a cake and have it.”
Kwa hiyo suala la Prof. Ibrahim
Haruna Lipumba kurudi kwenye nafasi ya Mwenyekiti wa CUF Taifa baada ya zaidi
ya miezi kumi ni wazo chelewefu (afterthought) na ndiyo maana amekua akiitika
wito wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa kama Mwalikwa kutoa maoni juu ya mambo
mbalimbali.
3) BAADHI YA WAJUMBE WA MKUTANO
MKUU MAALUM KUHITAJI PROFESA LIPUMBA AITWE KATIKA CHUMBA CHA MKUTANO KUJIELEZA.
Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la
The Civic United Front CUF limesikitishwa kwamba hujajielekeza kabisa juu ya
namna Prof. Lipumba alivyovamia Mkutano Mkuu Maalum wa Taifa wa tarehe
21/08/2016 akiwa na genge la wahuni ambao sio wajumbe wala waalikwa wa mkutano
huo (kama yeye) na wahuni hao wakiwa na silaha mbalimbali na kwa hiyo
tunachukulia kwamba unaunga mkono vitendo hivyo.
Ibara ya 117(2) ya Katiba ya CUF
haitoi fursa kwa kiongozi aliyejiuzulu kujieleza juu ya kujiuzulu kwake mbele
mkutano husika. Hata hivyo, umuhimu huo haukuwepo kwa sababu chama kiliridhika
kwamba ni yeye ndiye aliyejiuzulu na aliondoka ofisini na akaacha kutekeleza
majukumu yake ya Mwenyekeiti wa CUF Taifa.
Pia alikabidhi barua yake ya
kujiuzulu kwa mkono wake mwenyewe tarehe 05/08/2015 na siku iliyofuata ya
tarehe 06/08/2015 aliufahamisha umma kupitia vyombo vya habari kwamba
alijiuzulu na alithibitisha hiyo. Maelezo ya Profesa Ibrahim Lipumba yalikuwa
tayari yanafahamika kwa wajumbe wengi wa Mkutano na hakukuwa na suala jipya
kuhusiana na kujiuzulu kwake.
Hivyo haukuwa sahihi hata kidogo
kusema kuwa Profesa Lipumba alipaswa kujieleza mbele ya Mkutano Mkuu.
Msimamo wako huo ni kinyume na
Katiba ya CUF na hali halisi ilivyokuwa. Mashaka uliyojijengea kuwa huenda
barua iliyosomwa haikuwa yake hayana msingi wowote maana tangu mwaka 2015 ofisi
yako imekuwa ikifanya kazi na Chama cha CUF kupitia viongozi wengine na ukiwa
Mtanzania tunaamini ulipata taarifa za kujiuzulu kwake kwa njia nyingi. Ofisi
yako pia ilipokea taarifa rasmi kutoka CUF, kwa hiyo inashangaza sana kusikia
kuwa hata ofisi yako haikuwa na taarifa za kujiuzulu kwa Profesa Lipumba.
4). UHALALI WA KURA ZILIZOPIGWA
KUKUBALI AU KUKATAA PROFESA LIPUMBA KUJIUZULU.
Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la
The Civic United Front CUF linabaini tafsiri ya matumizi ya ibara ya 77(8) (d)
ya Katiba ya CUF ambayo tunapenda kuidurusu hapa chini:
“77(8) Kwa madhumuni ya kijifungu
cha (7) cha kifungu hiki, maamuzi muhimu ni pamoja na
(d) kuwasimamisha, kuwaachisha au
kuwafukuza uongozi na/ au uanachama viongozi wakuu wa Kitaifa wa Chama pamoja
na viongozi wengine wa Kitaifa kama ilivyoainishwa ndani ya Katiba hii.”
Kijifungu hicho hakihitaji tafsiri
yoyote na kiko wazi, kwamba matumizi ya kifungu hiki ni pale ambapo
yanajadiliwa masuala ya kuwasimamisha, kuwaachisha au kuwafukuza uongozi na au
uanachama viongozi wakuu wa Kitaifa wa Chama. Katiba hii haitoi wajibu wala
haifanyi suala la kujiuzulu Kiongozi wa Kitaifa wa Chama kuwa ni jambo muhimu
linalohitaji kupigiwa Kura kwa mujibu wa tafsiri yako. Ikiwa Lipumba angelikuwa
anasimamishwa, anaachishwa au kufukuzwa uongozi au uanachama ndipo matakwa ya
uamuzi muhimu kikatiba yangelifanyika.
Lakini Profesa Lipumba alijiuzulu
mwenyewe, hakusimamishwa, hakuachishwa na wala hakufukuzwa uanachama au uongozi
kwa hiyo Mkutano Mkuu wa CUF kikatiba hauwezi kushughulikia suala la kujiuzulu
kwa kiongozi kama uamuzi muhimu.
Tambua pia kuwa Katiba ya CUF ni
yetu wenyewe na wewe ni Msajili, tunaifahamu vyema sisi wanachama na viongozi
kuhusu maudhui yake kuliko wewe ambaye mara zote tunakupa taarifa baada ya
maamuzi ya vikao na Katiba hiyo kuwasilishwa kwako kwa usajili tu. Kujiuzulu
kwa Profesa Ibrahim Haruna Lipumba kulifanyiwa maamuzi kwa mujibu wa Ibara ya
115(1) ya Katiba ya CUF na siyo ibara ya 77(7).
Kura zilizotakiwa ni zaidi ya nusu
tu na siyo 2/3 (theluthi mbili) na kura zilizopigwa kubariki kujiuzulu kwake ni
476 ambazo ni asilimia 70 ya idadi ya wajumbe wote wa Mkutano Mkuu na kwa hiyo
maamuzi ya ibara ya 117 (2) yalifanywa kwa uhakika, kikatiba na bila shaka
yoyote.
Taarifa za vurugu wakati wa maamuzi
siyo ya kweli. Unatambua kuwa vurugu hizo zilitokea baada ya ajenda ya kukubali
kujiuzulu kwa Profesa Ibrahim Haruna Lipumba kukubaliwa na ajenda hiyo kufungwa
na mkutano kuahirishwa kwa mapumziko na kwamba baada ya mapumziko na wakati
mkutano uko kwenye ajenda ya pili ndipo vurugu zilitokea.
Hata hivyo, unatambua kuwa vurugu
hizo alizisababisha yeye mwenyewe Prof. Lipumba alipofahamu maamuzi ya Mkutano
na wakati wa Kuchagua Mwenyekiti mpya wa kujaza nafasi yake iliyoachwa wazi kwa
kujiuzulu.
5). UHALALI WA KIKAO CHA BARAZA KUU
LA LA UONGOZI LA TAIFA CHA TAREHE 28 AGOSTI 2016.
Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la
The Civic United Front CUF limebaini kuwa ofisi yako imetambua Kikao cha Baraza
Kuu la Uongozi la Taifa cha tarehe 28 Agosti 2016. Hatuna mashaka na mtazamo
huu kwani ndiyo ukweli.
6). MAMLAKA YA BARAZA KUU LA
UONGOZI KUCHUKUA HATUA ZA KINIDHAMU.
Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la
The Civic United Front CUF halina mashaka na utambuzi wako wa mamlaka ya Baraza
Kuu la Uongozi la Taifa kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya viongozi wa
Kitaifa wa Chama.
Tunakushauri kifungu ulichotumia
ukisome pamoja na vifungu vingine ambavyo ni Ibara ya 82(1) (m) na 83(1).
7). UTARATIBU WA KUCHUKUA HATUA ZA
INIDHAMU.
Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la
The Civic United Front CUF linapenda kukufahamisha kuwa taarifa ya Kikao cha
dharura ilikuwa sahihi na ajenda ilikuwa inafahamika kwa wajumbe wa Kikao kuwa
ni kujadili hujuma. Hata hivyo, tunakanusha tuhuma kuwa Maamuzi muhimu kwa
mujibu wa ibara ya 77(8) na 81(4) hayakufanyika kwa kuzingatia matakwa ya 2/3
ya wajumbe.
Utatambua kuwa maamuzi yote ya
Baraza Kuu la Uongozi la Taifa yanaweza kufanyika kwa maafikiano au kwa wingi
wa kura. Tunakushauri urejee Ibara ya 81 (3) ya Katiba ya chama ambapo hata
maamuzi muhimu yanahusika.
Tafsiri ya neno “Unanimously”
hayamaanishi “Consensus”. Tunajiridhisha kuwa neno Unanimously kwa muktadha wa
Chama chetu ni kuwa wajumbe wote walipiga kura na hakukuwa na mjumbe aliyepinga.
Hatukuwahi kupata taarifa za mtu yeyote aliyethibitika kuwa alinyimwa fursa ya
kupiga kura. Kama maamuzi yalifanyika unanimously, basi yalifanyika kwa wingi
wa wajumbe zaidi ya 2/3 kila upande. Katiba ilizingatiwa.
8. UTEUZI WA VIONGOZI WA KITAIFA
ULIOFANYWA NA BARAZA KUU LA UONGOZI LA TAIFA.
Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la
The Civic United Front CUF linapenda ufahamu kuwa ibara ya 101 inalipa Baraza
Kuu la Uongozi Taifa uwezo wa kuunda Kamati yoyote na hivyo kujumuisha uwezo wa
kuunda Kamati ya Uongozi ilipoona kuna haja hiyo. Kamati iliyoundwa ni halali
kwa ajili ya utekelezaji mzuri wa sera na itikadi za chama. Majukumu ya
Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Chama Taifa yana lengo la kusaidia
utekelezaji mzuri wa sera na itikadi za Chama, kwa hiyo majukumu ni yale yale
na siyo tofauti.
Kwa mantiki hiyo, Kamati zote mbili
yaani ile ya awali iliyokuwa chini ya Mwenyekiti Mhe. Wakili msomi Twaha Issa
Taslima na hii ya sasa iliyo chini ya Mhe. Julius Mtatiro zote ni halali kwa
mujibu wa katiba ya Chama. Ofisi yako ilipokea taarifa ya Chama na inayo
(ambalo ndilo jukumu lako) iliyokuwa ikikueleza kuundwa kwa Kamati ya Uongozi
ya awali iliyokuwa chini ya uenyekiti wa Mhe. Twaha Taslima ambayo hukuhoji
uhalali wake na uliitambua na hata kufanya kazi nayo ilipokuwa ikiwasiliana na
wewe. Haiwezekani uone na utambue uhalali wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa
kuunda Kamati ya Uongozi kwa kipindi cha Agosti 2015 hadi Agosti 2016 lakini
usione uhalali wa kuundwa Kamati ya aina hiyo hiyo iliyoundwa tarehe 28 Agosti,
2016.
9. UHALALI WA UTEUZI WA VIONGOZI WA
KITAIFA ULIOFANYWA NA KIKAO CHA BARAZA KUU LA TAREHE 28 AGOSTI 2026.
Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la
The Civic United Front CUF linapenda kusisitiza kuwa uteuzi ulikuwa halali kama
tulivyoeleza hapo juu. Kama ulivyoeleza wewe, utabaini kuwa mamlaka ya uteuzi
wa viongozi wa Kitaifa ni Baraza Kuu la Uongozi la Taifa na ndicho
kilichofanyika na ambacho ni msimamo wa Chama. Na hiyo ina maana kuwa msimamo
wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la CUF ni kuwa Ndugu. Julius Mtatiro, Ndugu.
Severina Mwijage na Ndugu. Katani Katani ndiyo wajumbe wa kamati hiyo ya
uongozi na wanatambulika kikatiba katika chama chetu kama Wajumbe wa Kamati ya
Uongozi hadi hapo chama kitakapochagua Mwenyekiti mwingine.
10). HITIMISHO
Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la
The Civic United Front CUF limejiridhisha kuwa katika taarifa yako fupi umeweka
hitimisho ambalo linatoa hukumu (judgment) badala ya kushauri au kutoa taarifa
kama ulivyoitaja.
Kama tulivyokwisha kueleza kwenye
utangulizi wa barua yetu na kwa kuzingatia Sheria ya Vyama vya Siasa Sura ya
258 toleo la mwaka 2015 na kwa kuzingatia hukumu ya Mahakama Kuu ya Tanzania,
Dar es Salaam, mbele ya Mhe. Jaji Mihayo ambayo tunaiambatanisha na barua hii
kwa taarifa, tafadhali tambua kwamba hukumu yako ni batili na haina mashiko
kisheria.
Kwa yale ambayo umetoa ushauri kwa
mujibu wa Katiba ya Chama chetu, Chama kina hiyari ya kuukubali au kuukataa
ushauri huo kwa kuzingatia misingi ya Katiba yake, Kanuni zake na kuhakikisha
haki sawa kwa wote inatendeka wakati wote.
Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la
The Civic United Front CUF linasisitiza kuwa maamuzi yaliyofanywa na vikao
halali vya Chama vya Mkutano Mkuu Maalum wa tarehe 21/08/2016 na Baraza Kuu la
Uongozi la Chama Taifa la tarehe 28/08/2016 ni halali na tunakusihi uyatambue
hivyo.
Tunakukumbusha na kukukusihi
usiruhusu Ofisi yako itumike vibaya kutuletea mitafaruku na migogoro isiyo ya
lazima katika Chama chetu na hata kusababisha uvunjifu wa amani kama
ilivyotokea Jumamosi, tarehe 24 Septemba, 2016 katika Ofisi Kuu ya chama chetu
Buguruni Dar Es Salaam. Ushauri huu unazingatia ukweli kuwa Msajili wa Vyama
Vya Siasa Tanzania ni mteule wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye
ni mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa. Nguvu ya Chama cha CUF
Tanzania inafahamika na hasa katika ushiriki wake na matokeo ya Uchaguzi Mkuu
wa Rais, Wabunge na Madiwani mwaka 2015.
Matukio yaliyojitokeza Zanzibar na
siasa za nchi hii ni lazima yazingatiwe wakati ukitekeleza majukumu yako ili
kuepuka kutumiwa vibaya na watu walioshiriki kuhujumu chama chetu na demokrasia
wakati wa uchaguzi mkuu wa 2015 na marudio yake 2016 kwa Zanzibar. Taarifa
tulizo nazo za malengo ya Profesa Lipumba kuhujumu siasa za Chama Cha Civic
United Front (CUF) na mahusiano ya Chama na taasisi nyingine zinajidhihirisha
katika matukio yaliyofanywa na Profesa Lipumba tarehe 21 Agosti 2016 (Ubungo
Plaza, Dar Es Salaam – kwenye Mkutano Mkuu Maalum) na tarehe 24 Septemba 2016
(wakati akitekeleza kwa nguvu kile anachokiita “kurudishiwa uenyekiti wake na
Msajili) baada ya barua yako tajwa.
Mwisho, Baraza Kuu la Uongozi la
Taifa la The Civic United Front CUF haliukubali ushauri wako kwa sababu umevuka
mipaka ya mamlaka yako uliyokabidhiwa na Sheria namba 5 ya Vyama vya Siasa ya
mwaka 1992, imekiuka miongozo ya mhimili wa Mahakama ambayo imekwishatolewa juu
ya mamlaka yako na unakiuka misingi ya katiba ambayo inamtaka kila mtu
aliyepewa mamlaka katika nchi yetu azingatie sheria za nchi.
Kwa sababu hiyo Baraza Kuu la
Uongozi la Taifa la The Civic United Front CUF linakujulisha rasmi kuwa, maamuzi
ya vikao halali vya chama kwa maana ya Mkutano Mkuu wa Taifa tarehe 21 Agosti
2016 na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la tarehe 28 Agosti 2016 yanabakia pale
pale na kwamba Profesa Lipumba siyo Mwenyekiti wa The Civic United Front CUF
Chama Cha Wananchi na kuwa, wanachama na viongozi wote waliosimamishwa na ama
kufukuzwa katika kikao cha Baraza Kuu la Uongozi la Taifa cha tarehe 28 Agosti
2016 wanaendelea kuwa chini ya maamuzi hayo hadi pale mchakato wa kikatiba wa
kuwasikiliza (kwa waliosimamishwa) utakapokamilika.
Hatua yoyote ile ya kutengua
maamuzi yoyote ya vikao halali vya chama chetu itafanywa na vikao husika vya
chama au vikao vya juu yake kama ambavyo katiba yetu imeelekeza na kwamba
hatutakubali Ofisi yako kutuamulia nani anapaswa kuongoza chama chetu kwa
wakati gani ama tujiongoze katika chama chetu kwa namna gani.
Tunawasilisha.
HAKI SAWA KWA WOTE
…………………………………..
MAALIM SEIF SHARIF HAMAD
KATIBU MKUU
NAKALA;
Prof. Ibrahim Haruna Lipumba
Kilongawima, Kunduchi,
Dar es Salaam.
Bwana Ridhiwani H. Kilala na
Wenzako wawili
Bwana Abdul Kambaya na Shashu
Lugeye.
No comments:
Post a Comment