Mahakama ya Wilaya ya Ilala
imemhukumu Seleman Manoti, kifungo cha miaka miwili jela kwa kupatikana na
hatia ya kujifanya usalama wa Taifa.
Hata hivyo, mahakama imetoa hukumu
hiyo bila mshitakiwa kuwepo mahakamani kutokana na kuruka dhamana kesi hiyo
ilipokuwa inasikilizwa.
Akitoa hukumu hiyo jana, Hakimu
Mkazi, Flora Haule alisema kuwa upande wa mashitaka, ulileta mashahidi wanne
kwa ajili ya kuthibitisha tuhuma hizo.
Alisema kutokana na ushahidi
uliotolewa, mahakama imeridhishwa na ushahidi huo na kwamba mahakama inamtia hatiani
mshitakiwa licha ya yeye kutokuwepo.
“Hati ya kumkamata mshitakiwa
itolewe na adhabu hii itaanza kutumika pindi mshitakiwa atakapokamatwa kwani
alitoroka akiwa na haki ya kusikilizwa,” alisema Hakimu Haule.
Wakili wa Serikali, Ester Kyara
aliiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa mshitakiwa iwe fundisho kwa wengine.
Inadaiwa kuwa Novemba 19, 2014
maeneo ya Kariakoo Msimbazi wilayani Ilala, mshitakiwa alijitambulisha kwa
Issaya Odelo na Charles Odinga kuwa Ofisa Usalama wa Taifa, kitu ambacho alijua
si kweli.
Katika hatua nyingine, kondakta
Ally Salum (23), mkazi wa Mwananyamala, amehukumiwa kifungo cha miaka mitano
jela baada ya kupatikana na hatia ya kuiba daladala.
Mbali na mshitakiwa huyo, Exavery
Kaunga (44) ambaye ni mlinzi na mkazi wa Kiwalani, Minazi Mirefu, aliachiwa
baada ya ushahidi dhidi yake kuwa na shaka.
Akitoa hukumu hiyo jana katika
Mahakama ya Wilaya ya Ilala, Hakimu Mkazi Mwandamizi, Juma Hassan, alisema kuwa
upande wa mashitaka ulileta mashahidi wanne kuthibitisha kosa hilo.
“Nimeridhika na ushahidi uliotolewa
na upande wa mashitaka, nakutia hatiani mshitakiwa kama ulivyoshitakiwa kwa
kutumikia kifungo cha miaka mitano jela,” alisema Hakimu Hassan.
Kabla ya kutolewa adhabu hiyo, Wakili
wa Serikali, Grace Mwanga aliiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa mshitakiwa
ili iwe fundisho kwa wengine. Hata hivyo, mshitakiwa alipoulizwa ni kwa nini
asipewe adhabu kali, hakujibu chochote na mahakama kutoa adhabu hiyo.
Washitakiwa hao walishitakiwa kwa
makosa mawili ya kula njama kutenda kosa ambapo inadaiwa kati ya Julai 5, mwaka
jana, washitakiwa walikula njama kutenda kosa.
Pia inadaiwa Julai 5,2015 pembezoni
mwa barabara ya Nyerere katika Kituo cha Mafuta cha Victoria, washitakiwa
waliiba gari lenye namba za usajili T 624 CSH aina ya Eicher mali ya Kampuni ya
White Swan.
No comments:
Post a Comment