
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel
amezindua jengo jipya makao makuu ya Umoja wa Afrika ambalo limepewa jina la
rais mwanzilishi wa taifa la Tanzania, Julius Nyerere.
Jengo hilo ambalo jina lake kamili ni Jumba la Amani na Usalama
la Julius Nyerere limejengwa kwa ufadhili kutoka Ujerumani.
Litakuwa makao ya idara ya Amani na
Usalama ya AU na litatumiwa pia na maafisa wa kutoa tahadhari ya mapema kuhusu
mizozo barani pamoja na kuratibu juhudi za kulinda amani za AU.
Ujenzi wa jumba hilo, ambalo ukubwa
wake wa sakafu ni mita 13,500 mraba na linaweza kutumiwa na wafanyakazi 360,
uligharimu euro 27 milioni.
Jengo hilo lina ofisi za kufanyia
kazi, vyumba vya mikutano vya kutumiwa na Baraza la Amani na Usalama, chumba
cha kuratibia shughuli, maktaba na vyumba vya shughuli za pembeni.
Mwalimu Nyerere, ambaye alikuwa
rais wa Tanzania hadi 1985, alikuwa mmoja wa viongozi waanzilishi wa Muungano
wa Nchi za Afrika (OAU) ambao sasa ni Umoja wa Afrika (AU).

Mwalimu nyerere Alishiriki sana
katika jitihada za kuendeleza bara la Afrika na kusaidia mataifa ambayo
hayakuwa yamepata uhuru kujipatia uhuru wake.
Mwalimu Nyerere alipigania sana
kumalizwa kwa ubabe wa Wazungu katika nchi za Rhodesia (sasa Zimbabwe), Afrika
Kusini, na taifa la Kusini Magharibi mwa Afrika/Namibia (sasa Namibia).



No comments:
Post a Comment