
CHAMA cha Wananchi (CUF) wilayani
hapa kimetoa tamko la kutomtambua Mwenyekiti wa Taifa, Profesa Ibrahim Lipumba,
na kwamba hakitampokea katika ziara yake.
Lipumba anatarajia kuanza ziara
mkoani Tanga kesho huku uongozi wa chama hicho ukisisitiza kutambua
uamuzi wa Mkutano Mkuu uliomwondoa madarakani na wa Baraza Kuu kumvua
uanachama.
Mwenyekiti wa CUF wa Wilaya ya
Tanga, Rashid Jumbe alitoa tamko hilo jana akieleza kuwa hawatakuwa tayari
kukaidi Katiba ya Chama chao na kwamba hawatampokea na hakuna maandalizi
yatakayofanyika kumpokea.
"Tumeambiwa Lipumba ana
dhamira ya kufanya ziara mkoani hapa. Sisi kwa uamuzi wa Baraza hatumtambui,
wala hatujaandaa maandalizi ya kumpokea.
“Wilaya za Korogwe na Muheza ndizo
zimesema atazitembelea, lakini sisi hatuko pamoja nao na watakaompokea
wataingia kwenye mgogoro mwingine kwa sababu hatambuliki," alisema
Jumbe.
Mwenyekiti huyo pia alizungumzia
mgogoro baina yao na CCM kutokana na sakata la umeya ambapo alisema
hatima ya mgogoro huo itajulikana baada ya mkutano mkuu unaotarajiwa kufanyika
Oktoba 29.
Alisema kutokana na sakata hilo
walitoa malalamiko kwa viongozi mbalimbali lakini hakuna hatua zozote
zinazoendelea, hivyo Kamati ya Utendaji iliwataka madiwani wa chama hicho
kutohudhuria kikao chochote cha Halmashauri hadi itakapotoa uamuzi.
"Tumetoa malalamiko yetu kwa
viongozi wa CCMna lengo letu ilikuwa tuonane na Rais lakini tulimpata
Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa aliyetwambia kuwa atalifanyia kazi, lakini sasa
tumeamua kupeleka malalamiko yetu kwa wenye chama na wao ndio watakaotoa uamuzi
juu ya mgogoro huo.
“Hivyo tumeitisha mkutano ambao
utakuwa na wajumbe 440 ambapo tuna imani kuwa tatizo letu litakwisha Oktoba
29,” alisema Jumbe.

No comments:
Post a Comment