Mjumbe wa UN Maman Sidikou amesema wanajeshi 18,000 wa kulinda
amani wa umoja huo ambao wamo nchini humo hawana uwezo wa kukabiliana na ghasia
kama hizo iwapo zitazuka.
Maandamano yenye umwagikaji wa damu yamekuwa wakishuhudiwa mara kwa
mara kufuatia hatua ya kuahirishwa kwa tarehe ya uchaguzi wa rais.
Upinzani unamtuhumu Rais Joseph Kabila kwa kujaribu kukwamilia
mamlaka hata baada ya kumalizika kwa muhula wake Desemba.
Watu kadha walifariki wakati wa maandamano ya kupinga serikali mwezi
jana mjini Kinshasa baada ya tume ya uchaguzi kusema haingewezekana uchaguzi
ufanyike Novemba.
Makao makuu ya vyama vitatu vya upinzani yalishambuliwa na
kuchomwa moto.
"Wadau kutoka pande zote wanaonekana kuwa tayari zaidi na
kutumia ghasia kutimiza malengo yao," Bw Sidikou, mkuu wa kikosi cha
kulinda amani cha UN kunachojulikana kama Monusco, aliambia baraza la usalama
la UN Jumanne
"Ingawa Monusco itafanya kila iwezalo kulinda raia,
haina uwezo wa kukabiliana na hatari zote zilizopo."
Aliongeza: "Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Congo imeingia kipindi cha hatari kubwa kwa uthabiti wake.
Kipindi kijacho kitakuwa kigumu sana, kuna uwezekano wa kufikia pahala ambapo
ghasia zitazidi."
DR Congo haijawahi kuwa na rais
aliyekabidhi madaraka kwa njia ya amani kwa mrithi wake tangu uhuru miaka 55
iliyopita.
Bw Kabila aliingia madarakani 2001
baada ya kuuawa kwa babake Laurent Kabila.

No comments:
Post a Comment