Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA) kimesema ni uongo na ni propaganda za wapinzani wao kwamba Waziri
Mkuu Mstaafu Edward Lowassa alimhonga Mwenyekiti Freeman Mbowe ili kupata
nafasi ya kugombea urais mwaka 2015.
Dkt. Mashinji ameyasema hayo
katika kipindi cha Kikaangoni kinachorushwa na kituo cha EATV kupitia
ukurasa wa facebook ambapo wananchi walikuwa wakimuuliza maswali ya papo kwa
papo naye anayajibu.
“Si kweli kwamba Mwenyekiti Freeman
Mbowe alimhonga Lowassa ili agombee urais kupitia CHADEMA , ni propaganda
zinazoenezwa na wapinzani wetu ili kuwadanganya wananchi” Amesema Dkt.
Mashinji.
Amesema Lowassa alijiunga na
CHADEMA kwa njia halali kwa mujibu wa taratibu za chama, na maamuzi ya kumteua
kugombea urais yalifanywa na vikao halali kuanzia ngazi ya Kamati Kuu hadi
Mkutano Mkuu.
Kuhusu sababu za CHADEMA
kumkaribisha Lowassa licha ya kumtaja miaka mingi kuwa alihusika na ufisadi,
Dkt Mashinji, hakutaka kulifafanua kwa undani, lakini aliishia kusema kuwa wao
walijiridhisha kuwa hakuwa na hatia yoyote na kwamba kama kweli alikuwa ni
fisadi, basi vyombo vya dola vingemchukulia hatua.
"Kama mtu kweli alikuwa ni
fisadi, kwanini hakuwahi kuchukuliwa hatua, hata kufikishwa mahakamani?,
nadhani hilo tuliache" Alisema kwa ufupi Dkt Mashinji.
Aidha Dkt. Mashinji amewataka
watanzania na wapenzi wa CHADEMA kufahamu kwamba chama hicho hakipo kimya bali
kinaendelea na mikakati ya kuhakikisha kwamba kinawafikia watanzania kwa
kuwatetea kwa kila hali kutokana na mambo yanayoendelea nchini.
No comments:
Post a Comment