Akiongea katika mkutano wa kampeni wa kumuunga mkono mgombea wa
chama cha Democratic Hillary Clinton, Bw Obama amesema haina maana kukemea
matamshi ya kudhalilisha ya Bw Trump kuwahusu wanawake bila kujitenga na
mgombea huyo.
Akihutubu Greensboro, North Carolina, Jumanne jioni, Rais Obama
alishangaa ni vipi wanasiasa wa Republican bado wanataka Bw Trump awe rais.
"Hali kwamba sasa kuna watu wanaosema: 'Sikubaliani kamwe
na hili, napinga hilo kabisa ... lakini bado tunamuidhinisha.' Bado wanafikiri
anafaa kuwa rais, hilo kwangu halileti maana," alisema.
Bw Obama alisema matamshi ya Bw Trump kuhusu wanawake hata
yanaweza kumfanya akose hata kazi ya dukani.
"Sasa unapata hali ambapo huyu bwana anasema mambo ambayo
hakuna anayeweza kuyavumilia hata kama mtu huyo angekuwa akiomba kazi (maduka
ya) 7-Eleven," alisema.
Bw Obama alikatizwa mara kadha akitoa hotuba na wapinzani wa Bi
Clinton lakini alionekana kutoathirika. Badala yake aliwajibu: "Hii ni
demokrasia. Hili ni jambo zuri sana."
Watu hao waliokuwa wakimzomea walitolewa nje na maafisa wa
usalama.
Maafisa wengi wakuu wa chama cha Republican, akiwemo spika wa
bunge la wawakilishi Paul Ryan ambaye ndiye afisa wa ngazi ya juu zaidi wa
chama hicho aliyechaguliwa, wameshutumu matamshi hayo ya Bw Trump ambaye
anaonekana akijigamba kuhusu kudhalilishwa kwa wanawake kwenye video.
Bw Trump hata hivyo amewashambulia vikali wanasiasa hao na
kusema ni wasaliti, na kwamba inakuwa vigumu kupambana nao kuliko hata
wanasiasa wa chama cha Democratic.
Amesema kwa sasa minyororo iliyokuwa imemfunga imeondolewa na
ataipigania Marekani kwa njia anayoitaka.
Mhariri wa BBC wa masuala ya Amerika Kaskazini anasema
kimsingi kwa sasa Bw Trump ni kama anaendesha kampeni yake kama mgombea huru.
Amedokeza kwamba uhasama
uliojitokeza kwa sasa utaendelea hata baada ya uchaguzi.
Kwenye kanda ya video ya mwaka 2005
iliyotolewa Ijumaa, Bw Trump anaonekana akieleza jinsi alivyojaribu kuomba
kushiriki ngono na mwanamke aliyeolewa pamoja na pia kutoa matamshi mengine ya
kuudhi kuhusu wanawake.
Karibu nusu ya maseneta, magavana
na wabunge wote 331 wa Republican wameshutumu matamshi hayo ya video na karibu
asilimia 10 wametoa wito kwa Bw Trump kujiondoa, kwa mujibu wa shirika la
habari la Reuters.

No comments:
Post a Comment