
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
ameikaribisha kampuni ya ujenzi ya Moladi Tanzania ielekeze nguvu zake Dodoma
ambako kuna mahitaji makubwa ya nyumba za watumishi.
“Natambua kuwa mnatumia teknolojia
ya kisasa na ujenzi wa nyumba zenu unachukua siku chache sana. Ninawaencourage
mje Dodoma ambako kuanzia Machi mwakani, watumishi wengi wataanza kuhamia
huko,” amesema.
Waziri Mkuu ametoa wito huo jana
mchana (Jumatano, Oktoba 12, 2016) wakati akizungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa
kampuni hiyo, Bw. Abeid Abdallah ambaye alifika ofisini kwake Magogoni, jijini
Dar es Salaam na kumuonyesha ramani ya nyumba za watumishi ambazo wanazitumia.
Waziri Mkuu alisema Mamlaka ya Ustawishaji
Makao Makuu Dodoma (CDA) ina maeneo ambayo imeyatenga rasmi kwa ajili ya
viwanja vya makazi na anaamini katika muda wa miezi miwili wanaweza kujenga
nyumba za kutosha watumishi wanaotarajiwa kuhamia katika awamu ya pili.
“Nimeangalia michoro yenu, nyumba
za vyumba vitatu vya kulala zina hadhi ya kukaa hata wakurugenzi; na watumishi
wa kawaida wanaweza kumudu zile za vyumba viwili vya kulala… ninawatia moyo
mwende haraka Dodoma na wale ambao wako serious wataleta maombi yao mara moja,” alisema.
Waziri Mkuu alisema amefarijika
kuona kuwa size ya ramani zao inatosha kwenye kiwanja cha ukubwa wa mita za
mraba 550 ambacho ni high density na watumishi wengi wanaweza kumudu kuvinunua.
Kwa upande wake, Mkurugenzi huyo,
Bw. Abdalla alimweleza Waziri Mkuu kwamba nyumba ya ukubwa wa vyumba vitatu vya
kulala, yenye sebule, jiko, stoo na choo inatosha eneo la mita za mraba 94 tu.
“Kati ya vyumba hivyo vitatu,
kimoja ni master, pia kuna sebule, chumba cha kulia na kibaraza. Hii inaanzia
shilingi milioni 35 hadi milioni 41 kutegemea na aina ya vifaa unavyoweka
kwenye umaliziaji. Lakini tukiongeza na servant quarter utalazimika kulipia
shilingi milioni 7 ambapo unapata vyumba viwili na choo na bafu ndani,” alisema.
“Kimsingi, ni lazima tutaweka
madirisha, milango, vyoo, masinki ya bafuni na jikoni, tiles (na mtu
anaruhusiwa kuchagua za China, Italy au Spain),” aliongeza.
Akifafanua kuhusu nyumba yenye
vyumba viwili vya kulala, Bw. Abdalla alisema nayo pia ina sebule, jiko, stoo
na choo kimoja na inatosha eneo la mita za mraba 54. Alisema nyumba hizo
zinaanzia sh. milioni 20 hadi 25 kutegemeana na aina ya vifaa vinavyowekwa
kwenye umaliziaji.
Alisema ujenzi wa nyumba moja
unachukua wiki sita na kama viwanja viko eneo moja au jirani, wanaokoa muda wa
siku tatu hadi tano kwa kila nyumba.
“Tunajenga ukuta kwa kumwaga
theluji isiyochanganywa na kokoto ambayo ni mchanganyiko wa saruji, mchanga na
kemikali. Inakauka baada ya saa saba na ukuta wetu ni imara mara nne zaidi ya
ukuta uliojengwa na tofali la zege.”
Teknolojia yetu inawezesha ukuta wa
nyumba nzima kukamilika ndani ya siku sita, nyumba zetu zinastahimili
matetemeko, vimbunga na ujenzi wake unapunguza gharama za ujenzi kwa asilimia
40.
Akizungumzia kuhusu upatikanaji wa
nyumba hizo, Bw. Abdalla alisema wana mikataba na mabenki kwa hiyo wanaweza
kujenga nyumba na kuziuza mara moja lakini pia wananchi wanaweza kuingia
mikataba na mabenki na kulipia kidogo kidogo katika muda maalum (mortgage).

No comments:
Post a Comment