
Katibu Mkuu wa Chama cha
Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, amemdhibiti mwenyekiti anayetambulika
na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Profesa Ibrahim Lipumba kwa kuandika
barua kwa benki zote ili kudhibiti ruzuku ya chama isipite kwenye mikono ya
kiongozi huyo.
Hatua hiyo imekuja siku chache
baada ya Msajili wa Vyama vya Siasa, kumtambulisha Prof. Lipumba Benki ya NMB
Tawi la Ilala akitaka apewe ushirikiano wa kufungua akaunti mpya ya chama.
Taarifa kutoka ndani ya CUF
zinasema kuwa juzi Maalim Seif, aliandika barua kwa benki zote kuzuia hatua
hiyo kwa kuweka zuio la mtu yeyote kufungua akaunti ya chama.
“Unajua hii vita si ya kitoto ni
mapambano yaliyopo ndani ya CUF lakini yana nguvu kubwa kutoka katika kila
pembe ya watu wanaochukia upinzani. Na pia wapo hata viongozi wakubwa wa dola
ambao kila siku wamekuwa wakifanya kazi ya kuivuruga CUF.
“Walitegemea lakini tangu jana
(juzi) Katibu Mkuu ameziandikia barua benki zote nchini kuzuia mpango wa
Msajili kutaka kuchepusha ruzuku ya chama na kwenda katika mikono ya Lipumba na
sasa nakala yake imepelekwa kwa Msajili wa Vyama,” alisema mtoa
habari wetu.
Hatua ya Profesa Lipumba kufungua
akaunti inatokana na barua aliyopewa na Msajili wa Vyama vya Siasa ya Oktoba 6,
mwaka huu iliyosainiwa na Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza
kwenda kwa Meneja wa Benki NMB Tawi la Ilala.
Katika barua hiyo yenye kumbukumbu
namba HA.322/362/14/104 inamtambulisha Profesa Lipumba kutakiwa kufungua
akaunti mpya ya The Civic United Front (CUF).
Siri ya Profesa Lipumba kutaka
kufungua akaunti mpya yenye jina la Chama cha Wananchi CUF inadaiwa kutolewa na
watumishi wa benki wa tawi hilo.
Prof. Lipumba ni Mwenyekiti wa CUF,
anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama Vya Siasa, huku chama chake kikiwa
tayari kimemfukuza uanachama.
Ofisi ya Msajili wa Vyama Vya Siasa
kupitia Sisty Nyahoza ilinukuliwa na vyombo mbalimbali vya habari ikikiri
kumtambulisha Profesa Lipumba kwa Benki ya NMB ili aweze kufungua akaunti hiyo,
hata hivyo ikikana kujua matumizi ya akaunti hiyo.

No comments:
Post a Comment