
Makamu wa Rais, Samia Suluhu
Hassan, amekiri kuwapo uhaba wa dawa na vifaa tiba katika
hospitali za Serikali nchini.
Amesema uhaba huo wa dawa ni
changamoto ya muda mfupi na Serikali inatafuta ufumbuzi wa haraka
kuwahudumia wananchi.
Alikuwa akizungumza Dar es
Salaam jana wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa wodi ya kina mama na
watoto katika hospitali zote za rufaa za Mkoa wa Dar es Salaam.
Samia alisema anatambua changamoto
zinazoikabili Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,
kwamba ni ukosefu wa dawa.
“Natambua katika hospitali zetu za
rufaa tuna changamoto ya vifaa tiba na dawa, lakini Serikali tunaifanyia
kazi kila mwananchi aweze kupata huduma hizo kama ilivyopangwa,”alisema.
Alisema idadi watu
wanaoongezeka katika Mkoa wa Dar es Salaam husababisha msongamano wa wajawazito
na watoto katika hospitali za Serikali na kuwafanya kina mama walale chini au
walale mbali na watoto wao.
“Kwa mujibu wa takwimu za hivi
karibuni, takriban wanawake 432 kati ya vizazi hai 100,000, hufa kila mwaka
kutokana na uzazi na asilimia 80 ya vifo hivyo husababishwa na ukosefu wa vifaa
tiba, umbali wa vituo vya afya, upasuaji wa huduma za dharura ya upasuaji kwa
wajawazito na kuongezewa damu.
“Kwa Mkoa wa Dar es Salaam peke
yake, kuna zaidi ya hospitali 42 zinazotoa huduma za dharura za uzazi kwa kasi
ya ukuaji wa jiji na bado Serikali inahitaji zaidi ya hospitali 30 ndani ya
miaka 10 ijayo,”alisema.
Kwa mujibu wa Samia, mradi wa
ujenzi huo utagharimu Sh bilioni 4.5 kwa hospitali tatu na kila hospitali yenye
ghorofa tatu na uwezo wa kuwekwa vitanda 150, itagharimu Sh bilioni 1.2.
Alisema Serikali imejipanga
kuhakikisha hospitali zote za rufaa zinaendelea kuimarishwa ili kutoa huduma
bora za afya ikiwamo afya ya mama na mtoto.

No comments:
Post a Comment