Chama cha ACT- Wazalendo kimemuomba
Rais John Magufuli kuunda timu ya wataalamu kupitia upya rasimu ya Katiba ya
Jaji Joseph Warioba na kuitisha mkutano mkuu wa kikatiba ili kuipitisha.
Chama hicho kilisema mchakato wa kura za maoni uanze upya ili kupata Katiba Mpya.
Hayo ni miongoni mwa maazimio
matatu yaliyotolewa na chama hicho kwenye mkutano wa siku moja wa kidemokrasia.
Akisoma maazimio hayo, Ofisa Habari
wa chama hicho, Abdallah Khamis alisema, “chama kimeazimia mchakato wa
kuandika Katiba Mpya uanze kwa kufanya marekebisho ya sheria ya kura ya maoni
na Sheria ya mchakato wa Katiba.”
Alisema, iwapo Serikali itaamua
kwenda na Katiba Inayopendekezwa iliyopo sasa chama hicho kitaipinga kwa
kufanya kampeni ya hapana kwenye kura ya maoni.
Alisema wakati mchakato wa Katiba
ukiwa umesimama, Baraza la Wawakilishi Zanzibar limepitisha sheria ya kutafuta
mafuta na gesi kinyume na matakwa ya Katiba ya Muungano ambayo inatambua
mafuta na gesi kuwa ni masuala ya muungano.
“Mkutano Mkuu wa Kidemokrasia
umeshauri kuwa chama kimwelekeze mbunge wake kuwasilisha bungeni hoja binafsi
ya kufanya mabadiliko, kwa kuondoa mafuta na gesi kama jambo la muungano ili
kuiwezesha Zanzibar kutafuta mafuta na gesi asilia bila vikwazo,” alisema.
Khamis alisema chama hicho
kimeazimia kufanya maadhimisho ya miaka 50 ya Azimio la Arusha Februari,
2017.
“Katika maadhimisho hayo chama
kifanye mkutano mkuu wa Kidemokrasia jijini Arusha na kutanguliwa na
Halmashauri Kuu ya chama kwenye ukumbi uleule ambao Tanu ilifanya na kuzaa
Azimio la Arusha mwaka 1967,” alisema.
Ofisa huyo alisema katika
maadhimisho hayo chama kimeshauriwa kuwa wataalamu wa ndani na nje waalikwe
kujadili mafanikio na changamoto za Azimio la Arusha katika miaka 25
iliyopita.
Pia, wataalamu watajadili madhara ya kutelekezwa kwa Azimio la Arusha mwaka 1992 huko Zanzibar.
Pia, wataalamu watajadili madhara ya kutelekezwa kwa Azimio la Arusha mwaka 1992 huko Zanzibar.
No comments:
Post a Comment