Kampuni ya Simba Motors imesema ina mpango wa kujenga kiwanda cha
kuunganisha magari aina ya pick-up ambacho kitaanza kuzalisha magari kabla ya
Desemba 30, mwaka huu.
Ahadi
hiyo imetolewa leo mchana (Jumatatu, Oktoba 10, 2016) na Mkurugenzi Mtendaji wa
kampuni hiyo, Bw. Jitesh Ladwa mbele ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katika
mazungumzo yaliyofanyika ofisini kwake Magogoni, jijini Dar es Salaam.
“Tumeamua kuunda magari aina ya
pick-up kwa sababu ya mahitaji makubwa yaliyopo nchini. Takwimu zinaonyesha
kuwa, kwa mwaka Tanzania inanunua magari ya aina hii zaidi ya 4,000. Katika
nchi za SADC mahitaji ni pick-up 35,000 kwa mwaka. Tutaanza na mtaji wa dola za
Marekani milioni 200 na tumeomba ekari 200 katika eneo la EPZ,” alisema.
“Eneo la kiwanda cha kuunganisha
magari peke yake linahitaji ekari 50, kwa hiyo tukiweka na yadi za kupaki
magari, eneo la viwanda vingine, eneo la kushusha na kupakia makontena
yatakayokuwa yakisafirishwa kwenda nchi jirani, ni lazima tutahitaji eneo kubwa
zaidi,” amesisitiza.
Amesema mradi huo wa majaribio,
utaanza kwa kutengeneza magari 20 kila mwezi na kwamba kazi ya utengenezaji
magari itaongezeka na kufikia 1,000 na baadaye 5,000 kwa mwaka.
Bw. Ladwa amesema uundaji wa magari
hayo aina ya Foton-Tunland utafanyika kwa ubia baina ya kampuni yao, SUMA-JKT
na kampuni Foton International ya China kwa kutumia teknolojia ya Kichina na
kwamba magari hayo yanayotumia 4-Wheel Drive, yana uwezo wa kupita kwenye
barabara za aina zote.
Kwa upande wake, akizungumza mara baada ya kulikagua
gari la mfano aina ya Foton-Tunland, Waziri Mkuu amesema anawakaribisha kwenye
uwekezaji huo hasa ikizingatiwa kuwa magari hayo yana uwezo wa kupita kwenye
maeneo ya vijijini ambako barabara zake siyo nzuri.
No comments:
Post a Comment