Wafuasi 22 wa Kundi la ‘Blue
Guard’ la Chama cha Wananchi (CUF) wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam wakikabiliwa na mashitaka manne
likiwemo la kukutwa na silaha za Jeshi la Polisi.
Washitakiwa hao ambao ni wakazi wa
Zanzibar walifikishwa mahakamani hapo jana na kusomewa mashitaka na Wakili wa
Serikali, Patrick Mwita mbele ya Hakimu Mkazi, Godfrey Mwambapa.
Mwita alidai, washitakiwa hao
wanakabiliwa na mashitaka manne ya kula njama, kuingilia majukumu ya kipolisi
kupitia genge la uhalifu pamoja na kukutwa na silaha pamoja na zana za Jeshi la
Polisi.
Akisoma mashitaka, Wakili Mwita
alidai, kati ya Septemba 20 na 25, mwaka huu kati ya Zanzibar na Dar es Salaam,
kupitia kikundi cha Blue Guard, washitakiwa na wenzao ambao hawakufikishwa
mahakamani walikula njama za kuajiri watu, wafanye kazi za kipolisi kinyume cha
Sheria ya Makosa ya Jinai.
Aliendelea kudai kuwa, washitakiwa
wakiwa wanachama wa kundi la Blue Guard waliwaajiri watu kwa ajili ya kufanya
kazi za Kipolisi kinyume na sheria.
Wakili Mwita alidai, Septemba 25,
mwaka huu katika eneo la Mwananyamala, Dar es Salaam, wakiwa na lengo la
kutenda kosa, washitakiwa walikutwa wakiwa na silaha kinyume cha sheria ,
ikiwemo visu vitano pamoja na mabomu ya machozi 10 kwa ajili ya kuyatumia
katika uvamizi.
Aidha, inadaiwa siku hiyo hiyo, Dar
es Salaam, washtakiwa walikutwa wakiwa na zana za Jeshi la Polisi ambazo ni
mabomu ya machozi yanayotumiwa na jeshi hilo katika majukumu yao.
Baada ya kusomewa mashitaka
washitakiwa hao walikana kutenda makosa hayo, hata hivyo Wakili Mwita alidai
upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kuomba wapangiwe tarehe nyingine
ya kutajwa.
Upande wa utetezi kupitia Wakili
Hekima Mwesigwa uliiomba Mahakama kuliondoa shitaka la tatu katika makosa hayo
kwa sababu lina upungufu wa kisheria kwa kutumia baadhi ya maneno kupotosha.
Hata hivyo, Wakili Mwita aliiomba
Mahakama kutupilia mbali maombi hayo kwa kuwa shitaka hilo halina upungufu
wowote badala yake wametumia lugha ya mkato.
Hakimu Mwambapa alisema baada ya
kupitia vifungu vya sheria, amebaini kuwa shitaka halina mapungufu kisheria
hivyo ametupilia mbali maombi.
Aidha, alisema washtakiwa hao
watapata dhamana endapo watatimiza masharti ya kuwa na wadhamini wawili wa
kuaminika watakaosaini hati ya Sh milioni mbili kila mmoja, pia wawasilishe
vitambulisho vyao mahakamani. Kesi itatajwa tena Oktoba 20 mwaka huu.
Washtakiwa ni Hamis Omary Said
(49), Said Mohamed Zaharan (57), Hamid Nassor Hemed (44), Nassor humud Ally
(25), Othman Humud Abdlaah (34), Swalehe Ally Swalehe (30), Hamis Hamis Haji
(46), Majid Hamis Juma (58), Mohamed Hamis Ally (34), Ramadhan Rashid Juma
(30), Juma Hamad Seif (21) na Masoud Iliyasa Fumu (29).
Wengine ni Jecha Faki Juma (40),
Mbaruku Hamis Bakari (31, Mohamed Alli Zuberi (43), Muhsin Ally Juma (27),
Mohamed Amir Mohamed (30), Ally Juma Salum (35), Juma Hajji Mmanga (26), Ally
Nassoro Ally (46), Haji Rashid Juma (32) na Juma Omary Hamis (28).
Kufikishwa mahakamani kwa
washtakiwa hao kunatokana na mgogoro unaoendelea ndani ya chama hicho. Septemba
28, mwaka huu, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro
alitoa taarifa za kukamatwa kwa wafuasi hao kwa tuhuma za kupanga njama za
kufanya fujo na kuchoma ofisi za CUF zilizopo Buguruni Ilala jijini Dar es
Salaam.
No comments:
Post a Comment