Licha ya baadhi ya viongozi wa
ngazi za juu wa Chama cha Wananchi (CUF) na wa Umoja wa Katiba ya Wananchi
(UKAWA) kutamka kutomtambua Profesa Ibrahim Lipumba kama mwenyekiti wa CUF,
Lipumba ameendelea kufanya shughuli za chama hicho ambapo jana ameteua
wakurugenzi wapya kwa madai ya kujaza nafasi za wakurugenzi alizotengua teuzi
zao juzi.
Miongoni mwa Wakurugenzi aliodai
Lipumba kuwateua ni pamoja na;
1.
Mkurugenzi wa Uchumi na Fedha -Thomas Malima
2.
Maftaha Nachuma - Mkurugenzi wa Mambo wa Nje CUF
3.
Zaynab Mndolwa -Mkurugenzi wa Haki za Binadamu
4.
Jaffari Mneke -Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi.
Hata hivyo, Lipumba amedai kuwa,
aliowateua watakaimu nyadhifa hizo hadi watakapothibitishwa na Baraza Kuu
la Uongozi Taifa la CUF.
Aidha, amedai kuwa Naibu Mkurugenzi
wa Mambo ya Nje atamteua kutoka Zanzibar hapo baadae.
Sambamba na hilo, alisema
wakurugenzi na manaibu wakurugenzi aliowateua baada ya mkutano mkuu wa chama
hicho uliofanyika Juni, 21, 2014 wataendelea na nyadhifa zao huku akitishia
kuwa, ikimbidi kufanya mabadiliko ya wakurugenzi hao hatosita kufanya hivyo.
Katika hatua nyingine, Lipumba
alitoa maagizo kwa Mkurugenzi wa Uchumi na Fedha CUF ambaye ndiye Katibu wa
Bodi ya Wadhamini kuitisha kikao cha bodi hiyo Oktoba 4,2016 ili ipewe taarifa
ya msimamo na ushauri wa Msajili wa Vyama vya Siasa Jaji Francis Mutungi kuhusu
mgogoro wa uongozi kitaifa wa CUF.
Lipumba alisema kuwa, amefanya
teuzi za wakurugenzi hao kwa mujibu wa katiba ya CUF ya mwaka 1992 toleo la
2014 ibara ya 90 (1) (f) ambayo inasema kuwa Mwwenyekiti Taifa atateua
Wakurugenzi na Manaibu Wakurugenzi kutoka miongoni mwa wajumbe wa Baraza Kuu la
Uongozi la Taifa au wanachama jasiri wa chama.
No comments:
Post a Comment