Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 31 Oktoba, 2016 ataanza ziara ya
Kiserikali ya siku mbili nchini Kenya kwa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Kenya
Mhe. Uhuru Kenyatta.
Rais Magufuli anatarajiwa kuwasili
katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta Jijini Nairobi majira ya
saa nne asubuhi na baadaye kupokelewa rasmi na mwenyeji wake Rais Kenyatta
katika Ikulu ya Nairobi ambako viongozi hao watafanya mazungumzo rasmi.
Pamoja na kufanya mazungumzo rasmi
na mwenyeji wake, Rais Magufuli atakwenda kutoa heshima katika Kaburi la Rais
wa Kwanza wa Kenya Hayati Mzee Jomo Kenyatta na pia anatarajiwa kuhudhuria
dhifa ya kitaifa aliyoandaliwa na mwenyeji wake Rais Uhuru Kenyatta Ikulu
Jijini Nairobi
Katika ziara hii Rais Magufuli
anatarajiwa kutembelea kiwanda cha maziwa cha Eldoville kilichopo Karen
Jijini Nairobi, na pia anatarajiwa kuzindua barabara mchepuko ya Southern
By-pass iliyopo Jijini Nairobi.
Barabara hiyo mchepuko ya Southern
By-pass ni moja kati ya miradi mikubwa ya barabara nchini Kenya, inaunganisha
maeneo mbalimbali ya Jiji la Nairobi kwa barabara za juu na chini na imejengwa
kwa lengo la kupunguza msongamano wa magari katika Jiji hilo.
Rais Magufuli anatarajiwa kumaliza
ziara yake tarehe 01 Novemba, 2016 na kurejea Jijini Dar es Salaam.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa
Mawasiliano ya Rais, IKULU
No comments:
Post a Comment