Bodi ya wadhamini ya Chama cha
Wananchi (CUF), imegawanyika vipande viwili kutokana na mgogoro wa uongozi
unaoendelea ndani ya chama hicho.
Kugawanyika kwa bodi hiyo kumekuja
siku moja baada ya Mwenyekiti wake, Abdallah Katau kutangaza kutomtambua
Profesa Lipumba, huku baadhi ya wajumbe wakipinga tamko hilo wakiliita ni
batili kwa mujibu wa katiba ya CUF.
Akizungumza na waandishi wa habari
jana jijini Dar es Salaam kwa niaba ya wajumbe wenzake, mjumbe wa bodi ya chama
hicho, Peter Malebo, alisema hawatambui tamko lililotolewa na mwenyekiti wao
kwani bodi hiyo inajiandaa kuwakutanisha mwenyeki wa chama hicho, Profesa
Ibrahim Lipumba na Katibu Mkuu wake, Maalim Seif Sharif Hamad ili kuweza
kutafuta suluhu ya mgogoro huo.
Alisema kutokana na hali hiyo,
watakaa na wajumbe wenzao na kujadili suala hilo kabla ya kuwaita viongozi hao
ikiwa ni pamoja na kujadili ushauri wa Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji
Francis Mutungi.
“Tutakaa na wajumbe wenzetu ili
tuweze kujadiliana mgogoro wa viongozi wetu pamoja na kupitia maazimio ya
Msajili wa Vyama Vya Siasa ili tuweze kupata hoja ya kuwahoji kwenye kikao
hicho.
“Lengo letu ni kuhakikisha kuwa
chama chetu kinarudi kwenye hadhi yake kama ilivyokua awali kuliko hivi sasa
ambapo kimegubikwa na mgogoro wa uongozi wa kitaifa,” alisema Malebo.
Alisema ikiwa watashindwa kupata
mwafaka wataitisha Mkutano Mkuu wa dharura ili waweze kuwaeleza wajumbe
wa mkutano huo hali ya chama na hatua za kuchukua.
“Kama mwafaka hautapatikana katika
kikao hicho, tutalazimika kuitisha Mkutano Mkuu Maalumu ambao pamoja na mambo
mengine, tutawaeleza mgogoro wa viongozi wetu ili wajumbe waweze kutoa uamuzi,” alisema.
Alisema Bodi ya Wadhamini wa CUF
inaundwa na wajumbe wanane ambapo kutoka upande wa bara ni watano na Zanzibar
watatu.
Aliwataja wajumbe hao kuwa ni
pamoja na Abdalah Katau, Peter Malebo, Ally Mbarouk, Amin Mrisha, Zacharia
Kwangu, Yohana Mbelwa na Dk. Juma Muchi.
Alisema mpaka sasa bodi hiyo
imegawanyika ambapo wajumbe kutoka Zanzibar wanamwunga mkono Maalim Seif huku
wale wa bara wakimwunga mkono Profesa Lipumba hali inayozidi kupandisha joto
ndani ya chama hicho.
“Kinachotutafuna ndani ya CUF
ni ubaguzi unaoonyeshwa waziwazi kutoka kwa viongozi wa Zanzibar jambo ambalo
limechangia kila mtu kuwa upande wake, lakini tutaitana na kujadiliana suala
hili ili tuweze kupata mwafaka,” alisema.
Alisema bodi hiyo inafanya kazi
ndani ya kipindi cha miaka mitano ambapo iliteuliwa mwaka 2011 na itamaliza
muda wake, Desemba mwaka huu.
Atoa onyo Chadema
Katika hatua nyingine, Malebo
aliwataka viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kutoingilia
mgogoro huo kwa madai hauwahusu.
Alisema, kitendo cha Mwenyekiti wa
Chadema, Freeman Mbowe kujitokeza hadharani na kudai hamtambui Profesa Lipumba
inaonyesha wazi kuwa ameshiriki kuongeza mgogoro ndani ya chama hicho.
“Mbowe haumhusu mgogoro wa viongozi
wa CUF, huu ni mgogoro wa ndani ya chama, tunamshangaa kujitokeza hadharani na
kudai hamtambui Lipumba, yeye ni nani ndani ya chama?, tunamuonya asirudie,” alisema.
Alisema, chama hicho kimejipanga
kupambana na watu wanaoingilia mgogoro wao wakati si wanachama wa chama hicho,
jambo ambalo limechangia kuendelea kuchochea vurugu hizo.
No comments:
Post a Comment