UMOJA wa Vjana wa Chama Cha
Mapinduzi (UVCCM), umelihimiza Jeshi la polisi nchini kutambua kuwa ujambazi,
wizi wa kutumia silaha na uporaji bado ni tatizo linalohitaji kushughulikiwa
kwa nguvu zote kama ambavyo nchi ilisimama na kutekeleza operesheni mbalimbali
za ukombozi.
Pia, umesisitiza kuwa usalama wa
raia na mali zao unahitaji kulindwa ili kuepusha vifo, hasara, unyang’anyi wa
mali na vilema vya maisha kutokana na matukio yanayoweza kuwakumba wasio na
hatia mijini na vijijini.
Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka
Hamdu Shaka, alieleza hayo jana alipomtembelea kumjulia hali majeruhi Said
Ally, Mabibo Hostel.
Saidi alijeruhiwa maeneo mbalimbali
ya mwili wake ikiwa ni pamoja na kutobolewa macho katika tukio wizi wa kutumia
silaha Buguruni mjini Dar es Salaam, Septemba mwaka huu.
Shaka alisema tatizo la uhalifu,
unyang’anyi, uporaji na ukwapuaji mali kwa kutumia nguvu na silaha, linahiaji
kutazamwa kwa kina na upana unaostahili na vyombo vyenye dhamana vinavyosimamia
usalama wa raia na mali zao.
Alisema kuna haja ya polisi kubuni
mbinu mpya za kukabiliana na makundi ya wezi, waporaji na majambazi kabla
hawajaleta madhara na hasara kama ilivyomtokea Said ambaye sasa
amesababishiwa ulemavu wa kudumu wa kutoona.
“Kila siku mbinu za uhalifu,
ujambazi, wizi wa kutumia nguvu na silaha hubadilika, jukumu la kupambana na
matukio hayo hatari ni la polisi kwa kushirikiana na raia wema, janga hili
likiachwa wananchi wataishi kwa mashaka na hawatajituma kujiletea maendeleo,”alisema Shaka.
Alisema ikiwa wananchi wanajituma
kwa bidii kutafuta fedha na kubuni miradi ya kiuchumi halafu majambazi na
wanyang’anyi wanapora na kumfilisi aliyetafuta ndani ya saa chache, hilo
linaweza kuwatia hofu mwananchi na wajasiriamali na kuwafanya washindwe
kujituma kikamilifu jambo ambalo litakuwa na madhara makubwa katika kuzalisha
mali na kukuza uchumi.
Akizungumza kwa masikitiko na
huzuni kubwa , Shaka alisema tamaa ya kupata utajiri kwa njia haramu kwa mtu
mmoja mmoja au kikundi, kumemsibaishia hasara ya maisha dhidi ya Said ambaye
kwa sasa amekoseshwa uwezo wa kuendelea kupiginia maendeleo yake ya kiuchumi na
taifa kwa ujumla.
“Ifike mahali tatizo la uhalifu,
ujambazi na uporaji lishughulikwe kama harakati za mapambano dhidi ya
maambukizi ya virusi vya ukimwi, ukoma na kifua kikuu, tukilipuuza tatizo hili
litaigharimu jamii na kuwaletea kadhia ya umasikini wananchi na Tanzania kwa
ujumla,”alieleza.
Kwa upande wake majeruhi Said
aliishukuru UVCCM kwa kuonyesha kumjali na kufika kumjulia hali kutokana na
janga lililomkuta na kumpa msaada huku akiwahimiza waendelee kuikumbusha
serikali isimuache kwa sababu amedhulumiwa utu wake na watu aliowatuhumu kuwa
ni majambazi bila ya hatia wala kosa lolote.
Said alisifu ujio huo wa ujumbe
kutoka Makao Makuu ya UVCCM Taifa ulioongozwa na Shaka, Mwenyekiti wa UVCCM
Mkoa wa Dar es Salaam Omar Matulanga na makatibu wa umoja huo kutoka wilaya
tano za mkoa huo.
Alisema akiwa kijana amefarijika
kutembelewa na vijana wenzake huku akiwahimiza wasimchoke kwa sababu sasa
amekuwa kipofu na hajimudu tena kimaisha.
“Endeleeni kuikumbusha serikali
yetu na wasamaria wema wasinisahau, nina nguvu, akili na maarifa ya kujituma
ili nizalishe ila nimedhulumiwa macho yangu na sina hakika kama nitaona kama
mwanzoni “alisema
No comments:
Post a Comment