Mwezi mmoja tangu Serikali iseme
usalama wa chakula ni kwa asilimia 123, jana Ofisi ya Waziri Mkuu imezitaka
wizara, mikoa na halmashauri kuchukua hatua za kukabiliana na tishio la njaa
ikiwamo kuzuia matumizi ya nafaka kutengeneza pombe.
Pia, ofisi hiyo ya Waziri Mkuu
imewataka wananchi kuhifadhi chakula baada ya Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA),
kutabiri kuwa kuanzia Oktoba hadi Desemba mwaka huu, maeneo mengi ya nchi
yatakuwa na mvua zitakazonyesha chini ya kiwango huku maeneo mengine yakikumbwa
na ukame.
Akizungumza jana, Mkurugenzi wa
Idara ya Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu, Brigedia Mbaazi Msuya alisema hali hiyo
itasababisha ukame na tishio la njaa katika baadhi ya maeneo ambayo hutegemea
mvua katika kilimo.
Msuya alisema kutokana na utabiri
wa TMA, wananchi wanashauriwa kulima mazao ya muda mfupi na yanayostahimili
ukame.
“Maofisa ugani wanatakiwa kutoa
ushauri kwa wananchi kuhusu mazao wanayotakiwa kupanda kwenye maeneo yao,” alisema.
Aliwataka wananchi kuweka akiba ya
chakula cha kutosha hasa kwenye maeneo ambayo yanapata mvua chini ya
kiwango.
Kaimu Mkurugenzi, Idara ya Usalama
wa Chakula wa Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, MaryStela Mtalo alisema idara
hiyo itafanya kazi ya uratibu, ufuatiliaji na ukusanyaji na kutoa taarifa za
chakula kwa wakati.
“Wakala wa Taifa Hifadhi ya
Chakula wanaelekezwa kununua na kuhifadhi akiba ya chakula cha kutosha ili
kukabiliana na upungufu unaotarajiwa katika baadhi ya maeneo,” alisema.
“Mikoa na Halmashauri zake
zisimamie na kuimarisha mifumo ya kuhifadhi chakula baada ya mavuno ili
kupunguza upotevu wa chakula na kuhakikisha chakula kinapatikana.”
Taarifa hii ya tishio la njaa
inapingana na ile iliyotolewa Septemba 8 na Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na
Uvuvi William Tate Ole Nasha kwamba Watanzania wasiwe na wasiwasi kuhusu hali
ya chakula nchini kwa maelezo kuwa kuna ziada ya chakula zaidi ya asilimia 123
ikilichozalishwa msimu uliopita.
Akizindua tovuti ya Wakala wa Taifa
Hifadhi ya Chakula (NFRA) mjini Dodoma, Naibu Waziri Ole Nasha alisema hali ya
chakula inaridhisha kutokana na ukweli kuwa uzalishaji wa chakula ni kwa
asilimia 100 hali ya utoshelevu wa chakula ni asilimia 101 hadi 120 hali
inayotafsiriwa kuwa kuna chakula cha kutosha kwa miaka mitatu hadi minne.
“Nawasihi Watanzania kutunza
chakula kilichopo ili kitumike sasa na baadaye, hali ya uwepo wa chakula
ndani ya nchi itaonyesha kuwa kuna usalama kwa wananchi na wanaweza kuendelea
na shughuli zao za kila siku,” alisema.
Pia ni tofauti na taarifa
iliyotolewa Jumanne iliyopita na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Chakula na
Mifugo Dk Florence Turuka kwamba wilaya 42 nchini zinakabiliwa na uhaba wa
chakula huku Mkoa wa Kagera ukikumbwa na baa la njaa na ukame.
Kutokana na ukame huo, ng’ombe waliokuwa wanauzwa kwa Sh 600,000 wilayani Karagwe sasa wanauzwa kwa Sh 20,000.
Kutokana na ukame huo, ng’ombe waliokuwa wanauzwa kwa Sh 600,000 wilayani Karagwe sasa wanauzwa kwa Sh 20,000.
“Licha ya kwamba ripoti ya dunia
inaonyesha hali ya chakula duniani ni mbaya, Tanzania kipo chakula na
kinatosheleza kwa kiwango cha juu cha asilimia 123,”alisema Turuka
wakati akizindua ripoti ya Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) kwa mwaka
2016 inayoonyesha kuwa dunia inakabiliwa na balaa la njaa kutokana na
mabadiliko ya tabianchi.
No comments:
Post a Comment