Jeshi la polisi limedai kwamba
limeua majambazi wawili hatari na kukamata bunduki tisa,
kati ya hizo SMG saba, shotgun moja na riffle moja, risasi 473 na magazini 16
baada ya majibizano ya risasi katika misitu ya Milima ya Usambara, Kijiji cha
Magamba wilayani Lushoto.
Katika majibizano hayo, pia polisi
walidai kukamata bendera zenye maandishi ya lugha ya Kiarabu, redio saba za
upepo na soksi za kuficha nyuso.
Kamishna wa Operesheni na Mafunzo
wa Polisi, Nsato Marijani alisema jana kuwa hiyo ilikuwa operesheni ya kuwasaka
majambazi waliovamia Chuo Kikuu cha Sekomu, wilayani humo hivi karibuni.
Alisema katika tukio hilo, askari
wawili walijeruhiwa kwa risasi. Marijani ambaye alikuwa katika milima hiyo
inayodaiwa kuwa ngome ya majambazi hao, aliwataja waliouawa kuwa ni Mudrick
Abdi (24) maarufu kwa jina la Osama, mkazi wa Mbagala Majimatitu Dar es Salaam
na Sultan Abdallah (24) mkazi wa Kiembesamaki, Zanzibar.
Alisema askari waliojeruhiwa
wanaendelea na matibabu na kwamba hawakupata madhara makubwa kwa kuwa walikuwa
wamevaa majaketi ya kuzuia kupenya risasi .
No comments:
Post a Comment