Wakala wa Usajili wa Biashara na
Leseni (BRELA) umetoa muda wa miezi miwili kwa wafanyabiashara wanaotumia
majina ya biashara pasipo kusajiliwa wafanye hivyo haraka.
Akizungumza na waandishi wa
waandishi wa jijini Dar es salaam jana, Ofisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Bw.
Frank Kanyusi alisema katika zoezi la kutoa elimu na kurasimisha majina ya
biashara na kampuni linaloendelea katika mikoa mbalimbali imebainika kuwa
wafanyabiashara wengi wanatumia majina ya biashara pasipo kuyasajili.
“Sheria ya majina ya biashara
inamtaka mfanyabiashara kusajili jina la biashara yake ndani ya siku 28 toka
aanze kulitumia,” alisema Bw.Kanyusi na kuongezea kuwa kinyume na hapo
atakuwa amevunja sheria ya majina ya biashara.
Alisema baada ya muda huo kupita,
patakuwa na msako nchi nzima ili kuwabaini wale wote wanaotumia majina ya
biashara pasipo kusajili na kuwafikisha katika vyombo vya sheria au kuwatoza
faini.
Alisema kuwa sasa usajili wa majina
ya biashara umerahisishwa kwani unafanywa kwa njia ya mtandao kwa kutembelea
tovuti ya wakala huo ambayo ni www.brela.go.tz ili kupata maelezo yote ya namna ya
kusajili jina la biashara.
Aliwataka wafanyabiashara wasiishie
kusajili tu jina la biashara bali pia waende katika Mamlaka ya Mapato (TRA) kwa
ajili ya kupata namba ya Mlipa Kodi (TIN) pia waendele katika halmashauri zao
kupata leseni ya biashara.
“Kwa kurasimisha biashara serikali
itapata mapato kwani wigo wa walipa kodi utaongezeka na pia itakuwa faida kwa
wafanyabiashara katika kujengewa mazingira bora ya kufanya biashara,” alisisitiza
Bw.Kanyusi.
Alisema BRELA imejipanga kuzunguka
mikoa yote nchini ili kutoa elimu juu ya urasimishaji wa majina ya biashara na
makampuni kwani imeonekana wananchi hawana uelewa wa kutosha juu ya umuhimu wa
urasimishaji.
Hadi sasa BRELA imefanya ziara
katika mikoa ya Mwanza, Mara, Geita na Simiyu na wiki hii watakuwa mkoani
Shinyanga kwa muda wiki moja katika kuhamasisha wafanyabiashara kurasimisha
biashara zao.
Alisisitiza kuwa ni lazima
kuhakikisha kuwa biashara zinarasimishwa ili serikali iweze kuwatambua walipa
kodi wake ambao watachangia pato la taifa na kuiwezesha Tanzania kuwa ya uchumi
wa kati ifikapo mwaka 2025.
No comments:
Post a Comment