WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
ameuagiza uongozi wa mkoa wa Lindi kuhakikisha wanawakamata na kuwachukulia
hatua watu wote wanaoharibu mazingira kwa kufyeka na kuchoma moto misitu kwa
sababu wanaharibu mazingira na kusababisha ukame.
Amesema mkoa huo upo hatarini
kugeuka jangwa na tayari vyanzo vingi vya maji vimeanza kukauka kwa sababu ya
uharibifu wa mazingira unaotokana na watu kufanya shughuli za kijamii kwenye
vyanzo vya maji.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo jana
Jumanne, Oktoba 18, 2016 wakati akizungumza kwa nyakati tofauti na wananchi wa
wilaya ya Ruangwa katika mikutano iliyofanyika kwenye vijiji vya Nanjaru,
Nachinyimba, Nambiranje, Mkaranga, Nandenje, Nachinyimba na Mandarawe.
Alisema wakulima wa ufuta
wanatakiwa kuendelea kutumia mashamba yao ya zamani na kuacha tabia ya kufyeka
misitu kila mwaka na badala yake waanzishe mpango wa upandaji miti ili kuepusha
taifa kugeuka kuwa jangwa.
“Vyanzo vya maji vimekauka kwa
sababu tumekata miti mingi. Mito yote iliyokuwa inatiririsha maji imekauka.
Viongozi wa mkoa hakikisheni misitu inalindwa na atakayekutwa analima kwenye
vyanzo vya maji akamatwe,” alisema.
Waziri mkuu aliongeza kuwa “Ukataji
miti huu unaoendelea katika maeneo yetu hakutosababisha kukosekana kwa
maji tu, bali hata mazao yatapungua. Jambo hili itasababisha njaa
katika vijiji vyetu, hivyo tuache kukata miti.
Waziri Mkuu alisema kwa sasa Serikari
inatumia gharama kubwa kuchimba visima virefu kutafuta maji. Amesema zamani
walikuwa wanachimba mita 20 au 30 wanakuta maji na gharama yake ilikuwa sh.
milioni 35, ambako kwa sasa wanalazimika kuchimba mita zaidi ya 150 kwa gharama
y ash milioni 75 kwa kisima kimoja.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa
Lindi, Bw. Godfrey Zambi,aliwataka watendaji wa kata na vijiji kuimalisha
ulinzi wa maeneo ya misitu na maji, na atakayeshindwa atachukuliwa hatua kali
za kisheria.
“Hatuko tayari kutengeneza jangwa
hivyo tutapamba na wale wote wenye tabia za kuchoma moto misitu au kulima
kwenye vyanzo vya maji,” alisema.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI
MKUU,
JUMNNE, OKTOBA
18, 2016
No comments:
Post a Comment