Neema Lema (33), mke wa Mbunge wa
Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema), amepandishwa kizimbani katika Mahakama
ya Hakimu Mkazi Arusha.
Alifikishwa mahakamani hapo
jana na kuunganishwa katika kesi ya tuhuma za kusambaza ujumbe unaomkashifu
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo.
Katika kesi hiyo ya jinai namba 351
ya mwaka huu, mshitakiwa mwingine ni Lema ambaye alifikishwa mahakamani hapo
Agosti 20 mwaka huu.
Mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa
Mahakama hiyo, Agustine Rwizile, Wakili wa Serikali, Blandina Msawa, aliiomba
mahakama kufanya marekebisho kwenye hati ya mashtaka kwa kumuongeza
Neema.
Akisoma mashtaka yanayomkabili
Neema, wakili huyo alidai Agosti 20 mwaka huu, jijini Arusha,
mshtakiwa alituma ujumbe kwa simu ya mkononi uliosema, ‘karibu
tutakudhibiti kama Uarabuni wanavyodhibiti mashoga’.
Neema anayetetewa na Wakili Sheck
Mfinanga, alikana kutenda kosa hilo na kupewa dhamana hadi Novemba 15, mwaka
huu, kesi hiyo itakapotajwa tena.
Wakati huo huo, Jeshi la Polisi
mkoani Arusha, lilimkamata na kumhoji Lema kwa tuhuma za kutoa lugha za
uchochezi dhidi ya Rais Dk. John Magufuli.
Akizungumza na waandishi wa habari
jana, Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo, alisema Lema alitoa
lugha hiyo wiki iliyopita katika mikutano halali aliyoifanya jimboni kwake.
“Tumemkamata Lema kwa kutoa lugha
ya uchochezi ambayo ni kinyume cha sheria.
“Baadhi ya maneno aliyotoa yenye
uchochezi ni pamoja na kusemaRais Magufuli akiendelea kugandamiza
demokrasia, taifa litaingia katika umwagaji wa damu, nchi hii inaandaliwa
kwenda katika utawala wa udikteta pamoja na kuwataka wananchi wawe tayari
kwa lolote na waache uoga kwa vile uoga ni dhambi mbaya kuliko
dhambi zote duniani.
“Baada ya kumhoji kuhusu maneno
hayo, tulimwachia kwa dhamana na sasa jalada lale liko kwa Mwanasheria wa
Serikali kwa ajili ya kuandaa hati ya mashitaka afikishwe mahakamani,” alisema Kamanda
Mkumbo.
No comments:
Post a Comment