Mwanaume mkazi wa Ilala, Siwema
Seif (40) amehukumiwa na Mahakama ya Mwanzo ya Ilala kwenda jela mwaka mmoja
kwa kumtolea lugha ya matusi na kumdhalilisha kimwili, Zainab Ramadhan ambaye
ni mama yake mzazi.
Akisoma hukumu mahakamani hapo
jana, Hakimu wa Mahakama hiyo, Matrona Luanda alisema ushahidi uliotolewa na
shahidi namba moja ambaye ni mlalamikaji, ulionesha kukosa shaka na kumtia
hatiani mshitakiwa.
Shahidi huyo alisema siku ya tukio
mshitakiwa alifika nyumbani kwao akaomba chakula akajibiwa kuwa kuna wali na
mshitakiwa akasema hataki wali bali anataka ugali na mama akamjibu asingeweza
kupika ugali na kumsisitiza Siwema ale wali.
Zainab alisema baada ya majibizano
hayo, mshitakiwa alimtukana matusi ya nguoni mama yake, huku akisema hawezi
kumzaa na kumkashifu, kwamba hana sehemu ya kumzalia huku akitishia kumwua
akiahidi kumtoa roho ndipo amjue yeye ni nani.
Kwa mujibu wa Zainab, alipoona
ugomvi na matusi umezidi aliingia chumbani mwake, na ndipo mlalamikaji
akamfuata na kumtukana huku akitishia kumwingilia kinyume cha maumbile.
“Baada ya hapo mshitakiwa
alinivamia na kunidhalilisha kimaumbile kwa mikono yake,” alisema.
Baada ya ushahidi wa mama huyo
dhidi ya Siwema, Mahakama ilitoa nafasi kwa kijana huyo kujitetea na Mahakama
ikamtia hatiani.
Karani wa mahakama hiyo, Blanka
Shao alisema kwa kuwa mshitakiwa alikuwa mkosaji wa mara ya kwanza na kitendo
alichokifanya ni cha kifedhuli tena haonyeshi kujutia, alishauri apewe adhabu
kali ili iwe fundisho kwake.
Hakimu Luanda alimhukumu kwenda
jela mwaka mmoja kwa kitendo alichomfanya mama yake mzazi.
Awali, ilidaiwa mahakamani hapo,
kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo Agosti 9 Ilala, mtaa wa Sophia Kawawa,
nyumba namba 10.
No comments:
Post a Comment