Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya
Dar es-Salaam limetoa tahadhari kwa wakazi wa kanda hiyo pamoja na wageni
kutoka nje ya mkoa wa Dar es Salaam kwamba kuna baadhi ya matapeli wanatumia
majina ya viongozi wa serikali kujipatia fedha kinyume na sheria za nchi.
Kamishna wa kanda hiyo, Kamanda
Simon Sirro wakati akizungumza na waandishi wa habari jana alisema kuwa
jeshi hilo hivi karibuni limepokea malalamiko kutoka kwa raia wa kigeni kuwa
kuna wahalifu wanalitumia jina la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda
kuwataka watoe fedha kwa madai ya kuwasaidia wanafunzi kupata vyuo nje ya nchi.
Alieleza kuwa, mnamo Oktoba mosi
mwaka huu raia wa china Marco Li mfanyakazi wa kampuni ya Group six
International alipigiwa simu na mtu aliyejitambulisha kama Makonda na kumtaka
atoe kiasi cha dola za kimarekani 3500.
Alisema tukio lingine lilitokea
Oktoba 6, 2016 mkurugenzi wa kampuni hiyo Jensen Huang aliitumia fursa hiyo
kumwomba mkuu wa mkoa huyo bandia kwamba amsaidie kumwidhinishia kuongezwa muda
wake wa kuishi nchini ambao ulikuwa umeisha, na kwamba mhalifu huyo alimtaka
atoe dola za kimarekani 7000 sawa na sh. Milioni 15.2.
Kamanda Sirro amewataka wakazi wote
wa Dar es Salaam na wageni kuwa makini na matapeli hao na wakiona dalili za
utapeli watoe taarifa katika vituo vya polisi kwa msaada zaidi ili wahusika
wachukuliwe hatua za kisheria.
No comments:
Post a Comment