Mchungaji Kiongozi wa
Kanisa la Maombezi (GRC) la Dar es Salaam, Anthony Lusekelo, maarufu Mzee wa
Upako, amekamatwa na polisi akituhumiwa kumfanyia fujo na kutishia kumuua
jirani yake.
Tukio hilo lilitokea juzi maeneo ya
Kawe wilayani Kinondoni, Dar es Salaam, kuanzia saa 11 asubuhi hadi saa tatu
alipochukuliwa na polisi wa Kituo cha Kawe.
Wakati wa tukio hilo, Mchungaji
Lusekelo alikuwa ameegesha gari lake barabarani kiasi cha kusababisha usumbufu
na foleni ya magari mengine.
Chanzo cha tukio hilo kinadaiwa ni
kulipiza kisasi kwa jirani zake hao wanaoishi katika nyumba namba KAW/MZN/1348,
ambao alidai wamekuwa wakimkebehi kuwa hafai kuwa mchungaji kwa sababu ya
ulevi.
Licha ya baadhi ya watu kumsihi
aondoke eneo hilo kutokana na hadhi yake, mchungaji huyo alikaidi, huku
akiendelea kuongea kwa sauti iliyofanana na mtu mwenye kilevi.
Baadhi ya maneno yaliyosikika
kwenye video iliyorekodiwa eneo la tukio hayaandikiki kwa kuwa si
ya kawaida.
“Mjinga wewe, mimi ni zaidi ya
askari na wewe ni mgambo, na si mgambo wewe ni raia tu.
“Umenitukana sana wewe mpaka leo
nimeamua kuloana na mvua, usitoe gari hapo mshenzi sana wewe, na nikikuona
mahali popote…, mshenzi kabisa, muangalie sana huyo,” alisikika
Mchungaji Lusekelo akiongea kwa sauti.
Baada ya kuongea maneno hayo,
ilisikika sauti ya mwanamke kutoka ndani ya uzio wa nyumba hiyo ikimjibu
mchungaji huyo: “Huwezi, aniangalie kitu gani.”
Hata hivyo, hata watu mbalimbali
walipomsihi aache kutoa lugha hizo za kejeli na aondoe gari lake lililokuwa
limesababisha foleni, alikataa akisema hataliondoa hadi atakapokuja Kamanda wa
Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Simon Sirro.
Baada ya purukushani hizo, polisi
kutoka katika Kituo cha Kawe walifika eneo hilo saa tatu asubuhi, wakamchukua
mchungaji huyo na kumpeleka kituoni.
Inadaiwa baada ya kufikishwa
kituoni hapo, mchungaji huyo alipimwa kiwango cha ulevi na kukutwa 131, ambacho
kinaelezwa kuwa ni kikubwa – ulevi wa kupindukia.
Ilipofika saa tano asubuhi,
mchungaji huyo alihamishiwa Kituo Kikuu cha Polisi (Central), ambako huko nako
inadaiwa alipimwa kilevi na kuonekana kushuka hadi kufikia 121.
Alipotafutwa Kamishna Sirro ili
kuzungumzia sakata la mchungaji huyo, alisema atalizungumzia leo katika mkutano
wake na waandishi wa habari.
No comments:
Post a Comment