Mtu mmoja anayehusishwa na vitendo
vya ugaidi, Azan Abubakary amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Dodoma
Mjini na kusomewa mashtaka yake.
Akiwa amevalia fulana ya rangi ya
bluu na kijani na suruali nyeusi na viatu vya matairi (maarufu kama katambuga),
alisomewa shtaka lake mbele ya Hakimu Mwajuma Lukindo.
Mshtakiwa huyo anashtakiwa kwa
makosa ya kufadhili ugaidi chini ya kifungu cha 13 cha sheria ya makosa ya
kuzuia ugaidi namba 21 ya mwaka 2002.
Ilidaiwa kuwa Mei 15, 2016
alimtumia fedha Mohamed Ibrahim kwa njia ya M-Pesa kiasi cha Sh 265,000 katika
namba +254 708104109 kwa ajili ya kufanyia ugaidi nchini.
Aidha Julai 22, 2016 Abubakary
alionekana eneo la Dodoma akituma fedha kwa njia ya M-Pesa kwa Mohamed Ibrahim
Sh 148,000 kwa ajili ya kufanya vitendo vya ugaidi.
Hakimu Lukindo alisema mshtakiwa hatakiwi
kujibu chochote kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri
hilo.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma
katika taarifa yake kwa vyombo vya habari imesema kwamba mtuhumiwa huyo
aliyefikishwa mahakamani ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) Kitivo
cha Afya na yupo mwaka wa pili.
Taarifa hiyo iliyosainiwa na
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa, mtuhumiwa alikamatwa
Nzega mkoa wa Tabora baada ya kugundulika kuwa anajihusisha na mtandao wa
ugaidi wa kundi la ‘Al Shabaab’ kutoka Somalia.
Kamanda alisema mtuhumiwa alikamatwa
kutokana na taarifa za Intelijensia ya Polisi katika masuala ya ugaidi.
No comments:
Post a Comment