BALOZI wa Umoja wa Ulaya (EU)
nchini Tanzania na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Roeland Van de Geer
amesema Tanzania ina haki ya kuamua kutosaini Mkataba wa Ushirikiano wa
Kibiashara na Jumuiya ya Ulaya (EPA) hadi itakapojiridhisha manufaa yake.
Alitoa kauli hiyo jana jijini Dar
es Salaam wakati akizungumza na vyombo mbalimbali vya habari kuhusu masuala
mbalimbali pamoja na kujibu maswali ya wanahabari hao.
Akizungumzia suala la Tanzania
kutosaini mkataba huo wa EPA, ambao nchi wanachama waliosaini hufanya biashara
bila kutoza kodi, Balozi Van de Geer alisema ingawa wasiwasi wa Tanzania kuwa
mkataba huo utadhoofisha juhudi za nchi za kufufua viwanda vyake, haoni kama kuna
ushindani kwenye hilo.
“Ingawa sioni ushindani unaohofiwa
na Tanzania kwenye soko la EPA, lakini uamuzi wake wa kutosaini ni haki yao na
nisisitize kuwa ni vyema Tanzania isisaini mkataba wowote ambao wana mashaka
nao hadi pale watakapojiridhisha umuhimu wake,” alisema Balozi
Van de Geer.
Aliongeza ni vyema nchi ikachukua
muda kujiridhisha badala ya kukimbilia kusaini, kwa sababu endapo baadaye
wataona mkataba huo hauna manufaa na huku wameusaini, watasononeka hivyo ni
vyema wakaupitia na kuona kama una maslahi kwao.
Awali, Septemba mwaka huu,
Mwenyekiti wa EAC, Rais John Magufuli alisema viongozi wote kwa pamoja
walikubaliana kupewa muda wa miezi mitatu ili Sekretarieti ya EAC iangalie na
kupitia masharti ya EPA kabla ya kusaini ili kila mmoja afaidike.
Hata hivyo, katika jumuiya hiyo ya
EAC, nchi ambazo tayari zimesaini mkataba huo ni Kenya, Rwanda na Uganda na
nchi zilizobaki ni Tanzania na Burundi.
Rais Magufuli alisema katika
kikao hicho, walibaini mambo 10 ambayo yanapaswa kuangaliwa kabla ya kufikia
uamuzi kwa maslahi ya nchi na wananchi.
Mwenyekiti alitaja mambo ya
kuangaliwa kuwa ni kwa namna gani nchi za EAC zitafaidika, njia gani itatumika
kuzuia bidhaa za kilimo na kulinda wakulima, usawa, makusanyo yatokanayo na
bidhaa zitakazoingizwa, Burundi itasainije huku ikiwa imewekewa vikwazo na EU,
kujitoa kwa Uingereza EU na athari zake, kukosekana kipengele cha kuruhusu nchi
nyingine kujihusisha na nchi za EAC kibiashara, kukosekana ushuru wa forodha na
kipengele cha nchi kujitoa pale inapoona haijaridhika na mkataba.
Rais Magufuli alisema mkataba huo
ukisainiwa kwa wakati huu, nchi wanachama zinaweza kuingia kwenye mtego mbaya.
Akizungumzia kujiondoa kwa
Uingereza kwenye EU, Balozi Van de Geer alisema EU bado iko imara na umoja huo
utaendelea kuwa miongoni mwa mataifa yenye uchumi imara duniani.
Kuhusu kiwango cha biashara baina
ya Umoja wa Ulaya na Tanzania kwa mwaka, Balozi Van de Geer alisema hivi sasa
mauzo yamefikia dola za Marekani bilioni mbili kwa mwaka huku akimsifu Rais
Magufuli kwa sera yake ya viwanda na kusema umoja huo unamuunga mkono.
Aidha, aliisifu Serikali ya Awamu
ya Tano kwa kujitahidi kuendesha nchi kwa kutumia vyanzo vya mapato vya ndani
kwa wingi, badala ya bajeti kutegemea wahisani wa nje.
“Tumeona juhudi za serikali kwenye
suala la bajeti ya sasa utegemezi wa wahisani kutoka nje ni chini ya asilimia
15 ya bajeti, ukilinganisha na awali ambapo bajeti kwa asilimia 40 ilikuwa
tegemezi kwa wahisani, tunaona mabadiliko, na hii inaifanya Tanzania kuondoka
kwenye nchi za kundi masikini zaidi duniani,” alieleza.
No comments:
Post a Comment