Kufuatia uchumi wa Tanzania kuzidi
kukua na kushika nafasi ya kwanza kwa ukuaji uchumi katika ukanda wa Afrika
Mashariki, pamoja na jitihada zake za kuifanya nchi kuwa na uchumi wa kati
kupitia viwanda.
Imechaguliwa kuwa mwenyeji wa
mkutano wa tatu wa kimataifa wa Chama cha Kampuni Ndogo na za Kati Ulimwenguni
unaotarajiwa kufanyika kuanzia Disemba 5 hadi 7, 2016 katika Ukumbi wa Mikutano
wa Mwalimu Julias Nyerere, jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Taasisi ya Sekta Binafsi
nchini (TPSF), Godfrey Simbeye amesema chama hicho huchagua nchi yenye uchumi
mkubwa kuwa mwenyeji wa mkutano huo na kwamba kuchaguliwa kwa Tanzania kuwa
mwenyeji wake, kunaashiria kuwa miongoni mwa nchi inayokuwa kiuchumi kwa kasi
barani Afrika.
“Tanzania sasa inaanza kuonekana
kuwa na hadhi, hali hii huenda inachangiwa na utendaji kazi wa Rais John
Magufuli, na itakuwa nchi ya tatu kufanyika mkutano huo unaokutanisha wadau na
wamiliki wa kampuni ndogo na za kati duniani,” amesema.
Amesema mkutano huo utasaidia
kampuni za ndani kujifunza namna ya kutoka katika kampuni ndogo kwenda za kati
na za kati kuwa kubwa.
Amesema pia TPSF itaitumia fursa
hiyo kutangaza kwa wageni fursa za uwekezaji zilizopo nchini.
“Mkutano huo pia utafungua milango
ya biashara sababu tunatarajia wageni zaidi ya 200 kutoka nje, watahitaji
malazi, chakula na hata bidhaa nyingine za ndani. Pia tutawaomba wahudhurie
katika maonyesho ya bidhaa za Tanzania yatakayoanza Disemba 7 hadi 11, 2016 ili
wajionee bidhaa zinazozalishwa nchini,” amesema.
Simbeye amesema kuwa, tafiti
iliyofanywa na serikali mwaka 2013 na kuchapishwa mwaka huu inaonyesha kuwa
kuna viwanda 49,000 ambapo 20,000 ni viwanda vikubwa.
“Uchumi wa Tanzania utajengwa na
viwanda hasa vidogo ambavyo vitaongeza idadi ya kampuni ndogo nchini, nchi
inapokuwa na kampuni nyingi fursa za kiuchumi pia huongezeka sababu zinaajiri
watu. Taasisi ya Sekta Binafsi itaendelea kutangaza fursa za biashara na
uwekezaji zilizomo nchini,” amesema.
No comments:
Post a Comment