Raia watatu wa China wamepandishwa
kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashitaka ya
kumteka na kumjeruhi raia mwenzao, Liu Hong.
Washitakiwa hao, Chen Chuw Bao
(34), Wang Yong Jim (37) na Zheng Pa Jin (40) wamefikishwa mahakamani hapo jana
na kusomewa mashitaka mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidi, Cyprian Mkeha.
Wakili wa Serikali, Hellen Moshi
alidai kuwa Oktoba 21, mwaka huu katika maeneo ya Palm Beach Ilala, Dar es
Salaam Wachina hao walimteka raia mwenzao wa China, Liu Hong ili kumuweka
kizuizini.
Alidai kuwa siku hiyo katika maeneo
hayo ya Palm Beach, washitakiwa walimshambulia Hong katika sehemu za mwili na
kusababisha apate maumivu ya misuli.
Baada ya kusomewa mashitaka Bao
alikiri kutenda makosa yote, huku Jim akikiri kosa moja na Jin alikana
mashitaka yote.
Wakili Moshi alidai kuwa amepokea
taarifa kutoka kwa Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Kipolisi Ilala, Dar es Salaam,
SSP Salum Ndalama akiiomba Mahakama isitoe dhamana kwa washitakiwa hao.
Wakili Moshi alidai SSP Ndalama
ametoa zuio hilo kwa kuwa washitakiwa hao ni raia wa China, pia hawana kazi
wala hati za makazi ya kudumu.
Aidha, kuna taarifa za kuaminika
kwamba washitakiwa hao na watuhumiwa wengine ambao hawajakamatwa wanapanga
njama za kujihusisha na vitendo vya kihalifu ukiwemo utekaji.
Alidai washitakiwa hao na wengine
ambao hawajakamatwa wana mpango wa kulipiza kisasi na endapo wakipata nafasi ya
kupewa dhamana, wanaweza kwenda kupoteza ushahidi.
Wakili huyo, aliongeza kuwa rai ya
SSP Ndalama ni kuwa, washtakiwa hao waendelee kubaki rumande hadi kesi hiyo
itakapoisha ili kumlinda majeruhi pamoja na ushahidi. Baada ya kueleza hayo,
Hakimu Mkeha aliahirisha kesi hiyo hadi Novemba 11, mwaka huu.
No comments:
Post a Comment