Chama cha Wananchi (CUF),
kimesema taarifa zinazosambazwa katika vyombo vya habari na mitandao ya
kijamii, kwamba Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad anataka kuhama chama
hicho ni za kupuuzwa kwa kuwa hazina ukweli.
Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar,
Nassor Ahmed Mazrui alisema hayo jana baada ya baadhi ya vyombo vya
habari kuripoti kuwa Maalim anataka kuondoka ndani ya chama hicho cha upinzani.
Alisema tangu kuibuka kwa mgogoro
ndani ya CUF na Mwenyekiti wao, Profesa Ibrahim Lipumba imekuwapo mikakati ya
kuwakatisha tamaa jambo ambalo halitafanikiwa.
Mazrui alisema wanaopanga mikakati
wamehangaika kila njia na wameonekana kukwama, hivyo kuibuka na mkakati wa
kumzushia Katibu Mkuu kuhama chama.
“Hivi unafikiria Katibu Mkuu
anaweza kuhama chama katika mazingira rahisi kiasi hicho? Hiki chama
amekipigania vya kutosha wataondoka wao,” alisema.
Naibu Katibu Mkuu huyo aliwataka
wana CUF kuendelea kutoa ushirikiano kwa Katibu Mkuu wao na kupuuza kauli za
watu ambao wamepoteza mwelekeo kisiasa.
Alisema CUF si chama kinachotegemea
mtu mmoja, na pia hakiko tayari kumpoteza Maalim kwa vibwagizo vya vibaraka wa
chama tawala, ambao hawataki kupigania mabadiliko nchini.
Aidha, kuhusu chama kuwa kimya
kuhusu madai yao ya ushindi katika uchaguzi wa Oktoba 25 mwaka jana, alisema
bado wanaendelea na mchakato huo na watatoa taarifa hivi karibuni kuhusu hatua
waliyofikia.
Mazrui alisema kila kitu kinakwenda
vizuri na kutaka wana CUF kuwa na subira katika kipindi hiki, kwani mambo
mazuri hayahitaji haraka.
Alisema ushirikiano wanaopata
kutoka jumuiya ya kimataifa ni mzuri hali ambayo inawapa matumaini ya
kuhakikisha kuwa haki inapatikana.
“Suala la madai ya ushindi wa
uchaguzi linakwenda vizuri, na naamini hatima yake itapatikana kwa busara, ni
vema wana CUF kuwa na subira,” alisema.
Jana katika baadhi ya magazeti
ziliandikwa habari zikimhusisha Maalim na kuhama CUF na kutajwa kutarajia
kuhamia vyama vya ADA-TADEA, AFP au ACT-Wazalendo, ambapo viongozi wa vyama
hivyo walikanusha taarifa hizo.
Hali kadhalika Katibu Mkuu huyo
alihusishwa na kutaka kujiunga na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi
(Ukawa).
No comments:
Post a Comment